HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wauguzi uliosababishwa na kuondolewa kwa wauguzi 60 waliokutwa na vyeti bandia vya elimu ya sekondari.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru alisema jana kuwa hali hiyo imeathiri zaidi vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), ambavyo vinahitaji zaidi wauguzi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa hao.
Alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, na kutaja sakata hilo kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo.
“Hospitali yetu imepungukiwa na baadhi ya wauguzi walioondoka wenyewe kwa kuwa na vyeti bandia,” alisema.
Pamoja na upungufu huo, aliwataka wauguzi wafanye kazi kwa kufuata maadili ya taaluma, kuwa na nidhamu na tabia njema na kuwaonya wachache wanaochafua taswira ya uuguzi.
Aliagiza kila muuguzi awe na kitambulisho cha kazi kwa ajili ya kutoa huduma na kuwataka waheshimu taaluma yao.
“Mnapaswa kutumia lugha nzuri kwa wateja wetu ambao ni wagonjwa, mtoe maneno yanayostahili ili kutowakwaza maana yanasemwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hawana lugha nzuri,” alisema Profesa Museru.
“Hivyo wauguzi mshiriki kuongeza mapato ya ndani ambayo yatakayosaidia kulipa baadhi ya madai na kuhusu suala la sare tunalifanyia kazi ili kila muuguzi apewe,” alisema Museru.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa Hospitali hiyo, Agnes Mtawa alisisitiza kuwa wauguzi wote wanatakiwa kuwa na leseni ya kazi.
Alisema kitambulisho hicho ndicho kitakachowawezesha kutoa huduma kwa wagonjwa na atakayekiuka, atakuwa hatarini kukabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh milioni tano.
Agnes alisema wauguzi wengi hufanya kazi bila leseni hali ambayo ni kinyume na sheria ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
“Hivyo sheria hii itachukua mkondo wake kwa kila muuguzi atakayekwenda kinyume, kwa kutokuwa na leseni ya utoaji huduma kwa wagonjwa,” alisisitiza Agnes.