SAKATA la Wanafunzi Vyuo Vikuu Kukosa Mikopo Kujirudia Tena Mwakani..Serikali Yawatengea Bajeti Kiduchu..!!!


BUNGE limeishauri serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) baada ya kubaini wanafunzi wengi watakosa fedha hizo mwakani kutokana na bajeti ndogo iliyotengwa.

Ushauri huo ulitolewa bungeni mjini hapa juzi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipokuwa ikiwasilisha taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Akiwasilisha taarifa hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, alisema wamebaini wanafunzi wengi watakosa mikopo mwaka ujao wa fedha licha ya kuwa na ufaulu mzuri.

Alisema mwaka huu wa fedha wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa ukamilifu lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuacha wengine 22,947 wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya Sh. bilioni 427.5 kutotosheleza mahitaji.

Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema mwaka ujao wa fedha HESLB imeombewa Sh. bilioni 427.5 (sawa na bajeti ya mwaka huu) ilhali ufaulu wa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka huu.

"Kamati inaona kwamba, suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu wenye sifa," alisema.

"Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB ili wanafunzi wengi zaidi wanaostahili waweze kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu."

Awali akiwasilisha hutoba kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha juzi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, alisema HESLB itatekeza mambo manne ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wanufaika wa mikopo ambao idadi yake hakuitaja, hata hivyo.

Alisema jambo la pili ni kuboresha vigezo vya utambuzi ili kuwezesha wanafunzi wasio na uwezo wa kiuchumi kupata elimu ya juu kupitia mikopo na ruzuku.

Waziri huyo alisema bodi hiyo pia itapunguza utegemezi wa kifedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa asilimia 35.

Alisema jambo la nne ni kitambua vyanzo vingine vya kuchangia mfuko HESLB na ufundi kwa ajili ya kukopesha wanufaika wengi.

"Nitumie fursa hii kuwataka wanufaika wote ambao hawajaanza kufanya marejesho kutekeleza wajibu huo mara moja ili kuepusha usumbufu wa kuchukuliwa hatua za kisheria," alisema.

Prof. Ndalichako alisema kuwa, katika mwaka huu wa fedha, HELSB imetoa mikopo kwa wanafunzi 122,374.

Katika mchanganuo wake, waziri huyo alisema wanafunzi 28,785 ni wapya ambao mkopo wao unagharimu Sh. bilioni 104.614 na wanafunzi 93,559 ni wanaoendelea na masomo ambao unagharimu Sh. bilioni 379.18.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad