Wachezaji Kelvin Naftali na Selemani Abdul waliofanyiwa vipimo vya damu na mkojo baada ya mchezo wa mataifa Afrika kwa vijana wenye miaka 17, kati ya Tanzania 'Serengeti Boys ' na Angola juzi, wamefuzu vipimo hivyo.
Afisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kuwa vipimo hivyo vilichukuliwa kama utaratibu wa kawaida wa mashindano huyo.
"Kanuni za mashindano kila mechi, lazima wachezaji wawili kwa kila timu lazima wapimwe.
Kwa mechi ya jana, vipimo hivyo vilifanyika kwa Nashoni na Abdul ambao baada ya dakika 30, majibu yalirudi kuwa wako safi na kama ingekuwa kinyume wangechukuliwa hatua za kinidhamu, " alisema Lucas.
Lucas alisema kuwa hata kwenye mchezo wa kwanza kati ya Serengeti Boys na Mali, wachezaji Dickson Job na Israel Mwenda nao walipimwa.
Wakati huohuo: Serengeti Boys imewasili salama mjini Port Gentil tayari kwa mchezo wa mwisho dhidi ya Niger utakaochezwa Jumapili.