SERIKALI Yadaiwa Bil. 70/-. za Chakula ..!!!


SERIKALI inadaiwa kiasi cha Sh. bilioni 67.7 na wazabuni mbalimbali wanaotoa huduma za chakula, uchapishaji na usambazaji vitabu shuleni, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali(Tamisemi), Seleman Jafo amesema.

Jafo alibainisha jumla ya deni hilo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bernadeta Mushashu aliyetaka kujua serikali inadaiwa kiasi gani na kwa miaka ipi na wazabuni hao na ni lini madai yao yatalipwa.

Akijibu swali hilo, Jafo alikiri kuwa wapo wazabuni mbalimbali ambao wanaidai serikali baada ya kuipatia huduma.

“Wapo wazabuni waliotoa huduma za chakula katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum za msingi na shule za bweni za sekondari, na wazabuni waliochapisha na kusambaza vitabu shuleni,” alisema Jafo.

Alifafanua kiasi cha Sh. bilioni 54.8 zinadaiwa na wazabuni waliotoa chakula na pia Sh. bilioni 9.9 ni wazabuni waliotoa huduma ya uchapishaji na kusambaza vitabu vya shule za msingi.

Jafo alisema madeni hayo ni yale yaliyojitokeza kabla ya serikali kuanza kutekeleza sera ya elimu ya msingi bila malipo.

“Kwa kutambua umuhimu wa kuwalipa wazabuni hawa, serikali kupitia Wizara ya Fedha imeshalipa jumla ya Sh. bilioni 13.2 hadi kufikia Mei mwaka 2016,”alisema.

Naibu Waziri huyo alisema wazabuni wengi ambao madai yao hayajalipwa hadi sasa wataendelea kulipwa kwa awamu kadri uwezo wa serikali na upatikanaji wa fedha utakavyokuwa.

Aliwaomba wazabuni hao kuwa wavumilivu kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati serikali ikiendelea kulipa madeni hayo ikiwa ni pamoja na madeni mengine ya ndani.

Akitoa jibu la nyongeza, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji alisema madeni hayo yanahakikiwa na mara baada ya uhakiki serikali hulipa.

Kufuatia kauli hiyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliagiza madeni yaliyohakikiwa yalipwe haraka ili kuwaondolea usumbufu wabunge ambao wamekuwa wakiandikiwa barua na wazabuni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad