SERIKALI Yaumwa Sikio Ripoti CAG..!!!


PROFESA wa Uchumi katika Chuo Kikuu Mzumbe, Honest Ngowi, amesema kuna haja ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha, kuongeza matumizi ya mashine za kieletroniki (EFD) na kutoa elimu sahihi kwa walipa kodi ili kuinua mapato.

Pia amesema kuwa mifumo ya usimamizi na utawala wa fedha iimarishwe pia na utaratibu wa misamaha ya kodi iangaliwe upya kuongeza ufanisi.

Prof. Ngowi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wadau wa haki na watetezi wa wananchi kutoka asasi mbalimbali ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenye ripoti ya mwaka 2015/16.

Alisema kwenye ripoti ambazo hutolewa mara kwa mara na CAG, pamoja na mapendekezo na maelekezo kutolewa na Kamati za Kudumu ya Hesabu za Serikali, hatua zinazochukuliwa bado hazijaleta mabadiliko kwa kiwango kikubwa.

“Kodi ikikusanywa ipasavyo huduma za jamii kama elimu, afya, miundombinu zitaboreka na hapa nidhamu katika matumizi ya fedha ni lazima,” alisema Prof. Ngowi na kuongeza:

“Ripoti inaonyesha kuna matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Mfano kuna magari 200 yamepewa msamaha kampuni mbili bila utaratibu. Haya ni matumizi mabaya ya misamaha na hivyo sheria ziangaliwe upya.”

Mkuu wa kitengo cha Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga, alisema uchelewaji wa fedha za miradi ya maendeleo inasababisha ufujaji wa fedha na mianya ya rushwa.

Alisema masuala yaliyojitokeza kwenye ripoti ya CAG, ikiwamo kukua kwa deni la taifa, kuwapo kwa watumishi hewa ambao walilipwa zaidi ya Sh. trilioni 1.4 pamoja na vyama vya siasa nchini kupata hati isiyoridhisha, yaangaliwe na kuchukuliwa hatua.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad