BAADA ya kushuhudia upinzani mkali kwenye kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la FA, ushindani na upinzani wa Simba na Yanga sasa umehamia kwenye michuano ya kimataifa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Yanga kufanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba ikikata tiketi ya kushiriki Kombe Shirikisho barani Afrika.
Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, aliliambia Nipashe jana kuwa kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika haitoshi na badala yake wanataka kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi.
"Lazima Simba ionyeshe utofauti... tunataka kurejea kwa kishindo kwenye michuano ya kimataifa kwa kuhakikisha tunafika mbali," alisema Mayanja ambaye juzi alikuwa pamoja na kikosi cha timu hiyo Bungeni mjini Dodoma.
Aidha, Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe akizungumza na Nipashe juzi, alisema ushiriki wa Simba na Yanga utaleta ushindani mkubwa kwao kwenye michuano ya kimataifa.
Alisema kila timu itataka kuizidi nyingine kwenye michuano ya kimataifa na hiyo itasababisha kujipanga zaidi kuelekea kwenye ushiriki wa michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
"Hii italeta changamoto kuhakikisha kila mmoja anamzidi mwenzake, michuano ya kimataifa ni migumu, lakini naamini maandalizi mazuri yanatoa msaada mkubwa kwenye kufanya vizuri," alisema Saleh.
Simba na Yanga zilionyesha mchuano mkali kuelekea mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kukabana koo hadi dakika ya mwisho kwa kufungana pointi 68 kila moja kileleni.
Hata hivyo, Yanga ilitangazwa mabingwa wa ligi hiyo kufuatia kuwa na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hapo mwakani.
Simba yenyewe ilipata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa Mbao FC mabao 2-1 katika mechi ya fainali ya Kombe la FA iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma Jumamosi iliyopita.
Katika kujiimarisha na michuano hiyo pamoja na Ligi Kuu Bara msimu ujao, klabu hizo kila moja imeanza kuendesha mkakati wa usajili kimyakimya, huku viongozi wao wakikataa kuweka wazi majina ya nyota wanaowahitaji.