WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Simbachawene amewahakikishia wabunge kuwa ahadi zote alizoziahidi Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 zitatekelezwa.
Simbachawene alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Hai(Chadema), Freemon Mbowe.
Mbowe alitaka kujua ni lini serikali itatoa Sh. bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita tano za lami ambazo Rais aliahidi wakati wa kampeni.
Akijibu swali hilo, Simbachawene alisema ahadi zote alizotoa Rais wakati wa kampeni zitatekelezwa ndani ya miaka mitano kama alivyoahidi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Salome Makamba, alitaka kujua ni lini serikali itatekeleza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa kampeni kwa wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini ya kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 10 za barabara za mitaa ya mji huo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Seleman Jafo alisema hatua ya kwanza ya utekelezaji wa ahadi ya Rais ilikuwa ni kuzitambua barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami katika Halmashauri ya mji huo ambayo imekamilika.
“Ujenzi huo utahusisha barabara ya Mama Farida yenye urefu wa kilomita 1.305, barabara ya Phantom-Majengo yenye urefu wa kilomita 1.852, barabara ya Nyihogo-Namanga yenye urefu wa kilomita 0.6,”alisema.
Alitaja barabara zingine kuwa ni barabara ya Florida-Stendi ndogo yenye urefu wa kilomita 0.829 na barabara ya Royal ya zamani-Stendi ndogo yenye urefu wa kilomita 0.2.
Alibainisha kuwa ujenzi wa barabara hizo utafanyika kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2017/18 na Sh. milioni 603.6 imetengwa kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilomita moja ya lami.
Aidha, alisema kupitia fedha za mfuko wa barabara zimetengwa Sh. milioni 320 kwa ajili ya kukarabati wa barabara za lami zenye urefu wa mita 800 katika mji wa Kahama.