WAKATI Dunia ikiwa imeaminishwa kuwa binadamu aliyeishi miaka mingi alikuwa anatoka nchini Italia na amefariki hivi karibuni, ameibuka mzee mmoja mkazi wa Kijiji cha Majengo, Kata ya Ihanda Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya ambaye ana miaka 127.
Mzee Ambilikile Mwanyaluke Panja, anaishi kitongoji cha Izyiga takribani kilomita mbili kutoka Kituo cha Mabasi cha Ihanda upande wa Magharibi, na hajiwezi kwa lolote kutokana na kuwa na umri mkubwa.
Kutokana na umri wake kuwa mkubwa ambao umemfanya kushindwa kutembea, familia yake inatumia kiti cha magurudumu kumsukuma wakati wa kumtoa nje na kumrudisha ndani.
Anasema Kabila lake ni Mndali na ni mzaliwa wa Kijiji cha Kapelekesi kilichopo katika Kata ya Kafule wilayani Ileje na kwa mujibu wa maelezo yake alihamia Mbozi baada ya vita ya kwanza ya dunia.
Baadhi ya matukio ambayo mzee Panja anayakumbuka ni pamoja na Vita ya Majimaji ya mwaka 1905 hadi 1907 ambayo anadai ilikuwa inapiganwa wakati yeye ana umri mkubwa na anachunga ng’ombe kijijini kwao Kapelekezi.
Mzee Panja anasema siri kubwa ya yeye kuishi miaka mingi ni aina ya vyakula alivyokuwa anakula tangu akiwa mtoto mpaka hivyo karibuni alipoanza kubadilishiwa.
Anasema alikuwa anakula zaidi ugali wa dona na wa Ulezi, ndizi aina ya Matoki huku mboga kuu ikiwa maziwa ya ng’ombe, maharage, Karanga na Njugu mawe.
Aidha anasema kipindi hicho kulikuwa hakuna chumvi za kisasa na badala yake walikuwa wanatumia chumvi za asili kwa kuchoma baadhi ya majani na kutumia majivu yake kwenye mboga (Chipembekwa).