MSAIDIZI wa kazi za ndani, Christina Mabuga (37), amekutwa amekufa ndani ya chumba chake, mwili ukiwa na majeraha ya kuchomwa kisu tumboni na shingoni dakika 25, tangu aachwe akiwa hai.
Taarifa kutoka eneo la tukio jana zilisema mwanamke huyo huenda alijiua kwa kuwa hadi mashuhuda waliofika kwanza nyumbani hapo walikuta milango ya nyumba hiyo ikiwa imefungwa na kuwalazimu kutumia mlango wa dharura.
Taarifa hizo zinaeleza kwamba tukio hilo lilitokea juzi mchana saa tisa alasiri, eneo la Moshi Bar, Ukonga Mombasa, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, mwajiri wa binti huyo, Anna Kasanda, alisema akiwa kazini alipokea taarifa majira ya saa tisa alasiri kwamba kuna matatizo yametokea nyumbani kwake.
Ndipo alipoanza kujiandaa kutoka ofisini na kurudi nyumbani, alisema.
Nyumbani hapo anaishi na shangazi yake ambaye alijua ya kwamba angeweza kutatua tatizo hilo ambalo hakuwa ameambiwa tayari, kabla ya yeye kufika kutoka kazini.
“Nilipopigiwa simu nilianza kujiandaa kuondoka kazini (muda huo huo) lakini nilifika nyumbani usiku," alisema Anna. "Nilipofika nikakuta baadhi ya majirani na watu wengine wakiwa wamejaa nyumbani."
"Nilipofika ndani nilianza kuona damu zimetapakaa na kuchuruzika kutoka chumbani kwa dada.
“Nilishangaa kwa kuwa nilipotoka asubuhi nilimuacha dada akiwa salama tu, ingawa kwa siku hiyo hakuonekana akiwa na furaha kama siku nyingine.
"Nilipoelezewa na majirani nikaambiwa mwili wa marehemu uliwahishwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, hivyo nikaukuta mwili huko.”
Alisema alipotoka nyumbani juzi asubuhi alimuacha binti huyo akiwa na shangazi yake ambaye hushinda nyumbani hapo muda mwingi, na kwamba mtoto wake alikuwa amekwenda shuleni.
Alisema muda wa kutoka shule mtoto wake ulipofika, shangazi alitoka mara moja na kwenda kumchukua mtoto njiapanda ya barabara, akimuacha binti huyo akiwa ndani.
"Shangazi alitumia muda wa dakika 25 hadi kurudi nyumbani na mtoto," alisema.
“Baada ya kurudi, alipofungua mlango wa mbele, ulikuwa haufunguki na alipojaribu kumuita dada kwa nje kwa muda mrefu tu ili amfungulie, hakukuwa na majibu yeyote.
"Ndipo alipoamua kuzunguka nyumba na kuchungulia dirisha la chumba cha binti huyo na kuona akiwa amelala chini na damu zikiwa zimetapakaa.”
Anna alisema baada ya shangazi yake kuona hivyo, alipiga kelele na kuwaita majirani ambao walimsaidia kufungua mlango wa dharura nyuma ya nyumba na kuingia ndani.
“Binti huyu nimekaa naye kwa zaidi ya mwaka mmoja... tumeishi vizuri tu na jana (juzi) wakati naondoka kwenda kazini aliniambia ya kwamba wazazi wake wamempigia wana shida na fedha hivyo nimpatie ili awatumie,nikasema sawa.”
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi, mwajiri huyo alisema na kwamba baada ya tukio hilo la juzi baadhi ya majirani walitoa maelezo Polisi.
Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamdan, alisema yuko safarini hivyo aulizwe kaimu kamanda wa mkoa huo.
Kaimu Kamanda wa mkoa huo, Ernest Matiku, alisema kuna taarifa kuhusu tukio hilo, ingawa yeye si mzungumzaji.
“Sawa, kuna taarifa hizo, ila mimi sio mzungumzaji kwa sasa,” alisema Matiku.