TANESCO Waeleza Chanzo Kukatika Umeme Mara kwa Mara..!!!


MVUA zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeathiri huduma za utoaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kusababisha kukatika kwake katika maeneo ya Tabata, Tandika, Kariakoo na Mbagala jijini Dar es Salaam.

Aidha, kutokana na uharibifu wa miundombinu ya barabara, mafundi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), walishindwa kufika kwa wakati katika maeneo yenye matatizo na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam kumekuwapo na tatizo la kukatika kwa umeme kwa  sababu hizo.

Alisema tatizo halipo katika miundombinu ya Tanesco bali ni tatizo la miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha kushindwa kufikika kwa urahisi.

"Kumekuwapo na tatizo katika baadhi ya maeneo kukosa umeme na changamoto ya kuchelewa kurudisha huduma hiyo kwa wakati inatokana na maeneo mbalimbali kuharibiwa vibaya na mvua. Ni vyema wananchi wakatoa taarifa haraka wanapoona tatizo badala ya kuanza kulitafutia ufumbuzi wenyewe… ingawa si rahisi kufika kwa wakati kutokana na hali ya hizi mvua," alisema Dk. Mwinuka.

Meneja Utekelezaji, Simon Kihiyo, alisema wakati huu wa mvua wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kutosogelea au kushika nyaya na nguzo zilizoanguka kwa sababu zinaweza kuleta madhara zaidi.

Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa mara tu wanapoona tatizo kwenye miundombinu ya Tanesco; kutotatua tatizo kwa njia ya mkato na kuwa makini na mifumo ya ndani ya nyumba zao.

Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji, alisema kuharibika kwa miundombinu ya maeneo ya tukio ndiko huathiri kufika kwa wakati katika maeneo yenye kuathirika.

"Kama tulikuwa tukifika eneo la tukio baada ya nusu saa basi kwa sasa tuna chukua muda mrefu kwa sababu ya hizi mvua, mafundi wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara zaidi," alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad