SEKTA ya viwanda imeanza kukua tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani na jumla ya miradi 393 yenye thamani ya Sh trilioni 5.198 inayotarajiwa kuzalisha ajira 38,862 imesajiliwa nchini.
Pia katika Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni jana, imeongezwa katika eneo la fedha za maendeleo na kufikia Sh bilioni 80 kutoka Sh bilioni 40 mwaka 2016/17.
Pamoja na hayo, katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilifanikiwa kusajili jumla ya miradi 242 ya sekta mbalimbali ikiwemo miradi ya viwanda 170 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 2,079 inayotarajiwa kutoa ajira mpya 17,285.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Alisema katika bajeti ya wizara hiyo imetengewa jumla ya Sh bilioni 122.2 kwa matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida ni Sh bilioni 42 na matumizi ya maendeleo ni Sh bilioni 80.1.
Tofauti na mwaka wa fedha unaoishia wa 2016/17, kiwango cha fedha kilichotengwa kwa wizara hiyo kilikuwa ni Sh bilioni 81.8 za matumizi ya kawaida na maeneo, kati ya hizo Sh bilioni 41.8 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 40 kwa ajili ya fedha za matumizi ya maendeleo.
Waziri huyo alisema miradi hiyo mikubwa 393 kwa sasa ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na mingine iko katika hatua za miwsho za kuanza uzalishaji. “Kati ya miradi hiyo TIC imesajili midair 224, Mamlaka ya EPZ miradi 41 na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imesajili miradi 128.
Pia Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo (SIDO) limeratibu uanzishwaji wa viwanda vidogo 1,843,” alisema. Alieleza kuwa kwa miradi 242 iliyosajiliwa na TIC pamoja na kuwepo kwa miradi hiyo 170 ya viwanda, miradi 54 ipo katika hatua ya ujenzi na miradi 17 imeanza uzalishaji.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana shughuli za uzalishaji viwandani zilikuwa kwa asilimia 7.8 ikilinganishwa na asilimia 6.5 mwaka 2015 na ukuaji huo ulitokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa za vyakula, vinywaji na bidhaa za tumbaku.
“Ukuaji wa sekta ya viwanda wa asilimia 7.8 ni juu ya wastani wa ukuaji wa pato la taifa wa asilimia saba kwa mwaka jana. Pia mchango wa sekta ya viwanda umekuwa na kufikia asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.2 mwaka 2015,” alifafanua.
Waziri Mwijage alisema kwa mwaka jana pekee sekta ya viwanda imetoa ajira 146,892 ikilinganishwa na ajira 139,895 zilizotolewa mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.1.
Alisema kutokana na sensa ya mwaka 2013, Tanzania ina jumla ya viwanda 49,243 ambayo asilimia 85.13 ni viwanda vidogo sana, asilimia 14.02 ni viwanda vidogo, asilimia 0.35 ni viwanda vya kati na asilimia 0.5 ni viwanda viwanda vikubwa.
“Hali hii si ya kushangaza kwa kuwa taswira ya Tanzania kuwa na viwanda vidogo sana vingi inajitokeza pia katika nchi karibia zote duniani kwa mfano, Japan viwanda vidogo na vya kati vinachukua takribani asilimia 99 ya sekta viwanda, Kenya asilimia 98, Ujerumani asilimia 99, Malaysia asilimia 97.3 na Canada asilimia 98,” alisema.
Alitaja baadhi ya viwanda ambavyo vimeanzishwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kuwa ni viwanda vya uzalishaji chuma, viwanda vya saruji, vigae, nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, vyakula, mbogamboga na matunda, maziwa na mafuta ya kula ambavyo vyote vina fursa kubwa ya kutoa ajira kwa Watanzania.
Alifafanua kuwa katika kuhamasisha mikoa kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda, jumla ya mikoa 13 imetoa taarifa ya kutenga maeneo hayo, ambapo baadhi ya mikoa hiyo ni Kigoma imetenga jumla ya ekari 451.46, Kilimanjaro ekari 53,033.16, Simiyu ekari 807.06, Shinyanga ekari 33,637.63 na Tanga ekari 33,788.62.
Bei ya vyakula Akizungumzia bei za mazao makuu ya chakula, alibainisha wazi kuwa bei ya mazao ya chakula kama vle mahindi, maharage, mchele, ngano, uwele, ulezi na mtama zimeongezeka kwa kiwango tofautitofauti.
Kwa upande wa mahindi gunia la kilo 100 bei yake imeongezeka kutoka Sh 59,873 msimu wa mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh 99,527 sawa na asilimia 66.23. Bei ya mchele kwa gunia la kilo 100 iliongezeka kutoka wastani wa Sh 177,340 msimu wa mwaka 2015/16 hadi kufikia Sh 191,289 msimu wa 2016/17, bei ya gunia la maharage la kilo 100 limeongezeka kutoka Sh 162,383 msimu wa 2015/16 hadi kufikia 178,101 sawa na ongezeko la asilimia 9.68.
Alisema kupanda kwa bei hiyo ya mzao kumetokana na kushuka kwa ugavi kutokana na uhaba wa mvua msimu wa kilimo wa 2016/17. Viwanda vilivyobinafsishwa Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 jumla ya viwanda 30 vilivyobinafsishwa vilifuatiliwa kati ya hivyo 18 vinafanya vizuri, vitatu vinafanya kazi kwa kusuasua na tisa vimefungwa.
Kufuatiliwa kwa viwanda hivyo kunafanya jumla ya viwanda kwa mwaka wa fedha 2015/16 hadi 2016/17 vilivyofuatiliwa kufikia 110. “Juhudi mbalimbali zimefanyika kushawishi wamiliki kufufua viwanda vilivyofungwa baadhi vimefanikiwa kuwa katika mchakato wa kufufuliwa na vingine bado wamiliki wake wanatafutwa.
Hata hivyo, kuna changamoto ya madeni makubwa ya mikopo ya benki inayowakabili baadhi ya wamiliki wa viwanda hivyo, wizara inaendelea kutatua changamoto hizo,” alisema.