Tumuunge Mkono Mhe.Rais kwa Kupigania Rasilimali za Nchi Zisipotee Lakini Tuzuie Wajinga Wachache ...!!!


Anaandika Malisa Godlisten 
Tumuunge mkono Mhe.Rais kwa kupigania rasilimali za nchi zisipotee lakini tuzuie wajinga wachache wanaotaka kubeba jambo hili kisiasa. Nimemsikia Polepole akiwalaumu watanzania na viongozi wa dini eti wamekaa kimya wakati rasilimali za nchi zikiibiwa.

Ndugu Polepole hajawatendea haki watanzania wala viongozi wa dini, anapaswa awaombe radhi. Hivi waliotuingiza kwenye mikataba mibovu ni viongozi wa dini? Polepole anasahau kuwa mikataba yote ya hovyo inayoliangamiza taifa hili imepitishwa na serikali ya CCM na kuungwa mkono kwa kura nyingi za NDIYO kutoka kwa wabunge wa CCM?

Kimsingi Polepole hana "moral authority" ya kujadili suala hili maana CCM yake na wabunge wake ndio waliotuingiza kwenye matatizo yote haya. Kikubwa anachoweza kufanya Polepole ni kuomba radhi kwa niaba ya chama chake, kwa serikali yake kuliingiza taifa kwenye hasara kubwa. Na sio kuwalaumu viongozi wa dini.

Viongozi wa dini hawatungi sera, hawapitishi sheria, hawana nguvu ya dola. Sasa wanalaumiwa kwa lipi? Yani uache kulaumu wabunge wa CCM waliopitisha sheria mbovu za madini, uje kulaumu wachungaji, mapadri na masheikh? Upuuzi gani huu?

Serikali ya Rais Mkapa ndiyo iliyopitisha sheria inayoruhusu mchanga kusafirishwa nje ya nchi. Kwahiyo kama ni kuibiwa tumeibiwa tangu wakati wa Mkapa. Lakini Mkapa hakuwa TLP wala TADEA. Alikua CCM. Na wabunge wa CCM ndio waliopitosha sheria hiyo kwa wingi wao.

Leo watu walewale waliopitisha utaratibu huo kwa makofi ya shangwe, ndio haohao wanaompigia makofi aliyetengua utaratibu huo. Unafiki.!!

Wabunge wa upinzani walipokataa kupitisha sheria ya madini kwa dharura walifukuzwa bungeni. Walipohoji kwanini sheria nyeti inayolinda rasilimali zetu ipitishwe kwa dharura wabunge wa CCM walizomea.

Waziri Muhongo akasimama na kuwadhihaki wanasheria wa madini kuwa hawajui kiingereza. Spika akawafukuza wabunge wa upinzani, wale wa CCM wakabaki ndani na kupitisha sheria hiyo kwa kura ya NDIYO. Leo watu walewale, wa chama kilekile kilichotuingiza kwenye matatizo badala ya kuomba radhi, wanaibuka na kuwalaumu viongozi wa dini. Huu ni wendawazimu.!

Serikali ya CCM na wabunge wake wametuingiza kwenye matatizo makubwa sana kama taifa. Rais anapochukua hatua tunapaswa tumuunge mkono kwa umoja wetu kama taifa. Rais anafanya kazi ya nchi, sio kazi ya CCM. Kama mnataka afanye kazi ya CCM jengeeni matawi aje kuzindua.

Viongozi wengi wa upinzani walipohoji mambo haya waliitwa wachochezi. Leo Rais anafanya yaleyale ambayo wapinzani walihoji then viongozi wachache wa CCM wanataka kujivika ushujaa. Ujinga wa kiwango cha lami.

Na hili la madini ni moja tu kati ya mengi ambayo serikali ya CCM imetuingiza kwenye matatizo. Huko kwenye utalii, maliasili, uvuvi, uwekezaji etc kuna mengi mazito kuliko haya. Kwa mfano Loliondo kuna mwekezaji amepewa kibali cha uwindaji lakini amegeuza eneo hilo kuwa sehemu ya nchi yake. Ukiingia ktk himaya yake network ya simu ya mitandao ya ndani inapotea na inasoma United Arabs Emirates.

Mwarabu huyo anadaiwa kuwafukuza wakazi wa eneo hilo ambao ni wamasai na kuwachomea nyumba zao na kuchoma mifugo yao. Pia amejenga uwanja mkubwa ambapo ndege hutua moja kwa moja huko mbugani na kubeba wanyama kwenda uarabuni bila kukaguliwa na mamlaka yoyote ya ndani.

Jambo hili limepigiwa kelele na wapinzani kwa muda mrefu lakini wakaitwa wachochezi. Lakini siku Rais Magufuli akiamua kumfukuza huyu mwekezaji, viongozi wa CCM watakua mstari wa mbele kumpongeza Rais, wakati CCM hiyohiyo na wabunge wake wamemlinda Mwekezaji huyo kwa muda wote huu.

Tuache unafiki kwenye masuala ya kitaifa. Polepole aache kuwalaumu viongozi wa dini, instaed akilaumu chama chake na wabunge wake wa CCM kwa kupitisha mikataba ya hovyo inayoligharimu taifa. Rasilimali za nchi hii sio za CCM, sio za CHADEMA sio za ACT. Ni za watanzania wote. Yoyote anayezitetea tutamuunga mkono bila kujali tofauti zetu za itikadi za vyama.!

Malisa GJ

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad