UDSM kuburuzwa mahakamani


Anadai hakuomba usajili moja kwa kwa moja chuoni hapo bali aliteuliwa kihalali na TCU 

Dar es Salaam. Mwanafunzi aliyefukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alphonce Lusako amewasilisha maombi Mahakama Kuu aruhusiwe kukishtaki chuo hicho kwa kumkatisha masomo. 

Manase aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya sheria alifukuzwa baada ya kufutiwa usajili Januari 26, pamoja na mambo mengine akidaiwa kusajiliwa kwa makosa kwa sababu aliwahi kufukuzwa chuoni hapo. 

Lusako anayewakilishwa na Wakili Jebra Kambole anaiomba Mahakama impe kibali cha kuishtaki UDSM na itoe amri kuzuia uamuzi wa kumfutia usajili. 

Maombi hayo yamefunguliwa chini ya hati ya dharura na yamepangwa kusikilizwa Mei 23 na Jaji Pellagia Khaday. 

Hii ni mara ya pili kwa Lusako kufukuzwa chuoni hapo, mara ya kwanza ni Desemba 13, 2011 akiwa mwaka wa tatu akidaiwa kuchochea mgomo. 

Hata hivyo, anadai alikuwa akipinga ufisadi katika Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa kusajili wanafunzi hewa na katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). 

Baada ya kukaa uraiani kwa muda mrefu, aliamua kuomba usajili TCU ili kuanza upya masomo. TCU ilimsajili na kumpanga UDSM kusoma kozi ya sheria. 

Baada ya kusoma muhula mmoja, alipewa barua ya kufutiwa usajili ikieleza alisajili kimakosa chuoni hapo kwa kuwa tayari alishawahi kufutia usajili. 

Katika hati ya kiapo mahakamani, anadai hakuomba usajili moja kwa moja UDSM bali aliteuliwa kihalali na TCU yenye mamlaka ya kutathimini maombi yake na kumpangia chuo. 

Anadai hakupewa haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa kanuni za haki asili kabla ya kufutiwa usajili kwa sababu zisizo halali. 

Kabla ya kuwasilisha maombi mahakamani, alidai kwa mara kadhaa aliiomba UDSM imrejeshe chuoni bila mafanikio. 

Lusako alijiunga na UDSM kwa mara ya kwanza mwaka 2009 akiwa amedahiliwa kusoma Shahada ya Biashara katika Uhasibu. 

Mwaka 2011 pamoja na wenzake kadhaa walifukuzwa na kufutwa katika mfumo wa elimu nchini wakidaiwa kuratibu mgomo wa wanafunzi UDSM. 

Katika mgomo huo, walikuwa wakipinga kurudishwa nyumbani wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokuwa wameshawasili vyuo vikuu vya umma kwa hoja kwamba bajeti haitoshi. Walihoji kuwapo mikopo hewa iliyokuwa ikiishia kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu. 

Baada ya kufukuzwa walikakata rufaa Baraza la UDSM wakiomba lirejee uamuzi wa chuo lakini baraza lilikataa maombi yao. 

Agosti 30, 2012 walishinda kesi baada ya Mahakama kutupilia mbali mashtaka dhidi yao na waliporudi chuoni, yeye na wenzake 11 waliokuwa wameshtakiwa, lakini chuo kilikataa kuwarejesha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad