GHARAMA za ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mbezi Luis, Jijini Dar es Salaam zinakadiriwa kuwa Sh bilioni 28.71 zitakazotolewa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Serikai za Mitaa(LAPF), Serikali imesema.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema). Kubenea alitaka kujua mradi wa kuhamisha kituo cha mabasi unatarajiwa kutumia kiasi gani cha fedha kutokana na ahadi ya serikali ya kuhamisha kituo cha mabasi cha Ubungo kukipelekea eneo la Mbezi.
Akijibu swali hilo, Jafo alisema hadi tayari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na LAPF imeanzisha kampuni ya ubia ya Mzizima Properties Limited itakayohusika na usimamizi na uendeshaji wa shughuli za kituo za kila siku. “Kazi inayoendelea ni kumtafuta mtaalam mshauri kwa ajili ya kuthibitisha usanifu wa mwisho wa kina wa mradi ili kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi,” alisema.
Hata hivyo alisema, gharama halisi zitajulikana baada ya usanifu wa kina utakaofanywa na mtaalamu mshauri. Naye Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), katika swali la nyongeza alitaka kujua ni lini kituo hicho kitakamilika ili kuondoa msongamano katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo akisema kipo kwenye hali mbaya. “Kituo hiki kinajengwa pembeni ya barabara ya Morogoro na siku chache zilizopita Wakala wa Barabara (Tanroads) umetoa notisi kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo mita 121 kwa upande zote mbili kubomoa majengo yao ndani ya siku 28, ni kwanini serikali isitengue agizo hili ili majadiliano kwanza yafanyike,” alihoji.
Akijibu maswali hayo ya nyongeza, Waziri Jafo alikiri kuwa muda wa utekelezaji wa mradi huo umepita na kwamba, kuna ushauri umetolewa na Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa kuhusu mradi huo. “Pia Jambo hili ni suala linalohitaji fedha nyingi na wastani wa Sh bilioni 28 siyo jambo dogo kuna makubaliano yalifanyika kati ya Jiji na LAPF, na Mfuko umewahakikishia kuwa utatengeneza kituo ambacho kwa Dar es Salaam ni kikubwa na kitakuwa na uwezo wa kuchukua magari mengi,” alisema. Alifafanua kuwa kuhusu utekelezaji asiwe na wasiwasi utatekelezwa na kuhusu uvunjaji serikali itaangalia nini kifanyike kwa mstakabali wa wananchi hao.