UKWELI Mchungu ..Wasiposhtuka… Naliona Kaburi la Bongo Fleva Kama Bongo Muvi..!!!


SEHEMU yoyote kunapokuwa na ushindani, kunakuwa na maendeleo chanya. Kila mtu hujaribu kufanya mambo ‘unique’ ili kumfanya kuwa na mvuto zaidi kwa kile anachokifanya. Lengo kuu huwa ni kuteka hisia za watu juu ya bidhaa inayokwenda sokoni au kwa mlaji.

Kunapokuwa hakuna ushindani, watu huchoka kula bidhaa ya aina moja. Matokeo yake ni anguko.

Hicho ndicho kilichojiri kwenye Bongo Muvi kulipokuwa na ushindani mkubwa wa mastaa wawili, marehemu Steven Kanumba na Vincent Kigosi ‘Ray’. Hapana shaka kuwa, kuondoka kwa Kanumba kuliua ushindani na matokeo yake ni kama ulivyosikia. Bongo Muvi inaaminika kuwa tuendako kama hakutakuwa na mabadiliko makubwa basi kaburi hilooo…

Wakati kelele zikiwa nyingi kwenye Bongo Muvi na kila mmoja akisema lake, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, kama Bongo Fleva nako hakutakuwa na mshtuko au kuzinduka, basi nako kuna kishindo cha kifo kinafuata. Nitafafanua na kutoa tahadhari ya nini kifanyike ili tuendako kuwe salama.

Miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na shoo nyingi mno zilizosababisha kumbi za starehe na viwanja mbalimbali vya burudani kufurika hadi pomoni. Wakati fulani kumbi zilijaa hadi kukawa na tatizo la hewa kukata.

MTAZAMO WA MWANA-FA 
Kinachotokea sasa ni kwamba shoo hizo hakuna tena. Katika mazungumzo yangu na wanamuziki wakubwa wa Bongo Fleva kwa nyakati tofauti, kila mmoja alieleza dhamira yake ya kwenda kimataifa zaidi isipokuwa Hamis Mwinjuma  ‘Mwana-FA’ ambaye anaamini kwamba bado mashabiki wake wa Bongo na Afrika Mashariki wanamuhitaji zaidi kuliko huko kwingine.

Atakapoamini kuwa amekata kiu yao, automatic, hali itamlazimisha kwenda kimataifa kutokana na mahitaji na wakati.

KWA NINI SHOO ZA NYUMBANI ZIMEKATA? 
Uchunguzi huo ulibaini kuwa, wasanii wenyewe wanaamini kuwa, shoo za nyumbani za kuwaweka karibu na mashabiki wao, ambao kimsingi ndiyo waliowapa sapoti hadi kufikia hapo walipo, hazilipi na kwamba hazina mashiko! Nakataa!

Wengine wanasema hakuna wadau wanaondaa shoo hizo na kwamba wenyewe au msanii mmojammoja hawezi kuandaa shoo yake mwenyewe bila wafadhili, makampuni, mapromota na wadau wengine.

Wanachoshindwa kujua ni kwamba, mashabiki wao wa nyumbani waliowapa sapoti na majina makubwa, wanahitaji kuwaona wakiwaburudisha kwa namna yoyote ile bila kujali sababu au visingizio wanavyovitoa. Wakiwa-puuza, basi ndiyo kwaheri ya kuonana!

ZIKO WAPI SHOO ZA WIKI-ENDI?
Kama nilivyoeleza awali, miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na ‘events’ au shoo nyingi za kila wikiendi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Kumbi za burudani au klabu za usiku zilisheheni mashabiki wao.

Ulikuwa ni msisimko wa hali ya juu kwani mbali na kuwaona, kulikuwa na ushindani wa nani anayejua kutawala jukwaa na nani anayetoa shoo nzuri kuliko mwingine! Kwa sasa hilo halipo na ni vigumu mno kusikia msanii fulani ndiye mkali stejini kwa sasa.

NAY YUPO TOFAUTI 
Katika mazungumzo yangu na Mwanamuziki Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, yeye anaamini kuwa ndiye msanii pekee ambaye yupo karibu zaidi na mashabiki wake kwani huwa hajali kama ni wikiendi au ni siku ya kawaida kwani hugonga shoo nyingi zaidi hasa mikoani, wilayani na kwenye miji midogo vijijini.

Siyo kwamba hataki kuwa kimataifa, la hasha! Lakini bado anaamini kuwa mashabiki wake waliomkuza na kumpa jina kubwa wanahitaji burudani kutoka kwao na tena kwa viingilio vya chini kabisa vinavywawezesha watu wake wa hali ya chini kuhudhuria.

Na kiukweli kwa kufanya hivyo, Nay anakimbiza mwizi kimyakimya kwani anazichanga tu mdogomdogo.

KURUDISHA KWA JAMII NI TATIZO 
Kosa lingine kubwa linalofanywa na wanamuziki hawa ni kutorudisha fadhila kwa jamii. Tunaishi kwenye jamii zenye matatizo mengi kuanzia magonjwa, mazingira, uchumi mbaya na matatizo mengine ya msingi.

Ni nadra sana kumuona msanii akianzisha au akiwa mstari wa mbele kwenye kampeni ya janga fulani au kuhamsisha jamii kuondokana na janga hilo. 
Siyo lazima kutoa fedha nyingi, lakini kuonesha mashabiki kuwa yupo pamoja nao katika maisha yao ya kila siku.

Hili wanaliona ni jambo dogo lakini ni kubwa mno kwa mashabiki wao. Kwa msanii yeyote anayejitolea kwa jamii, hata anapopata tatizo hasa la ugonjwa akihitaji kuchangiwa, huwa ni ishu ndogo. Lakini kwa yule asiyekuwa karibu na watu wake huwa ni shughuli nzito. Mifano ipo mingi.

NINI KIFANYIKE KWA HARAKA KUNUSURU KIFO? 
Nimefungua mjadala huu mpana kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya huko tuendako yasiwakute ya Muziki wa Dansi, Taarab na yale tunayoshuhudia kwenye Bongo Muvi. Kwa mtazamo wangu, ni muda muafaka sasa kwa mastaa wa Bongo Fleva kuanza kuwa ‘selfish’, yaani wang’ang’anie kwanza kuwaridhisha mashabiki wao wa nyumbani, waliowanyanyua kabla ya kukimbilia shoo za nje ambazo mara nyingi wenyewe hukiri kuwa hazina masilahi zaidi ya sifa kwamba wanakwenda kufanya shoo ughaibuni.

Mfano mzuri ni msanii Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ambaye uchunguzi ulionesha kuwa hajafanya shoo kwa mashabiki wake wa Bongo au mkoani kwake, Kigoma tangu mwaka uanze.

Mastaa wa Bongo Fleva lazima wakubali kuwa wamekuwa hapo walipo kwa sababu ya sapoti waliyopewa nyumbani hivyo wawape burudani. Ni lazima waamini katika kurudisha kwa jamii, bila hivyo Bongo Fleva hiyooo…kaburini!

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad