UKWELI Mchungu..Linna Acha Kuigeuza Bongo Kuwa Marekani..!!!


Na JOSEPH SHALUWA

NAMFAHAMU Linna Sanga, mmoja wa wasanii mwenye uwezo mkubwa kwenye Bongo Fleva. Linna yumo kwenye listi yangu ya wasanii wa kike wanaojua wanachokifanya wakishika kipaza sauti.

Sina shaka hata kidogo na namna anavyoweza kucheza na sauti yake awapo jukwaani. Anaijua sauti yake ya dhahabu ilivyo, hivyo anaitumia vyema.

Ni miongoni mwa wasanii wachache wa rika lake, waliotoka pamoja na wakaendelea kuwepo kileleni hadi leo. Huwezi kusema amechuja! Utapigwa mawe. Ni msanii mkali, anayejua kujiongeza.

Kwa sasa msanii huyu mwenye figa bomba na kiuno chepesi awapo jukwaani, anapiga mzigo chini ya Kampuni ya Drops Up Entertainment ya jijini Dar es Salaam.

Singo yake ‘Raha Jipe Mwenyewe’ inadhihirisha namna anavyozidi kukua na kuujua muziki vizuri zaidi. Kwa maneno mengine, Linna anathibitisha ni kwa namna gani wasanii waliopitia THT walivyo bora na wanaojua muziki.

Niseme tu kwa kifupi na kwa lugha iliyonyooka, Linna ni msanii mzuri, mwenye kujua kipaji chake na kukitumia sawasawa. Vijana wa sasa tunasema, anakitendea haki.



SIDE B YAKE SASA

Side B ya Linna inaanza kuharibu heshima yake kwa jamii. Linna mwenye sifa zote nilizotaja, ameondoa utu wake na kufanya jambo la kipuuzi, akiigia Wazungu ambao tamaduni zetu na zao ni tofauti.

Sitaki kuzungumzia sana kuhusu historia yake ya mahusiano, lakini naweza kusema kuwa hana sifa mbaya inayoweza kumuweka kwenye kundi la wasichana wasiojielewa.

Amekuwa akijiheshimu na kutulia na anayekuwa naye kwenye uhusiano, tena kwa uwazi kabisa. Siyo msichana waluwalu kwenye uhusiano. Kwa sasa anatoka na mkurugenzi wa Drops Up Entertainment, inayosimamia kazi zake.

Tatizo ni baada ya uhusiano wake wa sasa kuzaa kitu cha tofauti na uhusiano mwingine aliopitia huko nyuma. Linna ni mjamzito.

Aliwahi kusema kuwa anajisikia fahari kupata ujauzito na kwamba ni kitu alichokuwa akikisubiria kwa muda mrefu – swadakta kabisa!

Lakini tatizo ni pale alipoanza kusambaza picha zinazomwonyesha baadhi ya sehemu za siri za mwili wake. Upuuzi huu nani alimshauri?

Namfahamu Linna, nimewahi kukutana naye mara kadhaa kikazi na hata kirafiki. Siyo jambo la ajabu kwa kazi yangu, lakini kwa hili sina haja ya kukupesa macho, namweleza kwa uwazi kabisa amebugi!

Kuacha tumbo nje, kuvaa kanguo ka ndani tu na kutundika picha kwenye mitandao ni kujidhalilisha. Ni kuwavunjia heshima wazazi wake na ndugu zake.

Ni kuwakebehi mashabiki wake. Ni ujumbe mbaya kwa jamii. Linna mwenye historia nzuri hata ya makuzi yake kiimani, anawezaje kufanya ujinga wa namna hii?

Tangu lini Watanzania tukawa hivyo? Mwili wa mwanamke wa Kiafrika husitiriwa. Mwanamke wa Kitanzania asili yake ni kujihifadhi, siyo kuonyesha sehemu zake za kujihifadhi hadharani.

Katika hili Linna amepotoka na anastahili kuomba radhi kwa wadau wake ambao kwa muda mrefu wamemuheshimu na kumuunga mkono kwenye shughuli zake za muziki.



ANANGWA MITANDAONI

Wadau walipoona picha za staa huyo, wakamnyoosha! Wakamkumbusha kuwa siyo sahihi kwa kueleza maoni yao. Wengi wameonyesha hasira zao, kwamba alichofanya siyo sahihi.

Tatizo ni namna alivyopokea. Akiwajibu mashabiki wake, Linna alisema eti alichofanya ni jambo la kawaida na kwamba yeye si wa kwanza kufanya hivyo.

Eti kwa Linna, kuanika tumbo na kutokea akiwa na nguo ya ndani nje ni Uafrika! Eti kwa sababu picha zenyewe zina mwonekano wa weusi zaidi ni jambo linalomwakilisha Mwafrika.

Maajabu haya! Mwafrika anakaa utupu? Leo hii Linna anataka kuturudisha nyuma, eti anasema asili ya Mwafrika ni kuvaa majani au ngozi sehemu ya mbele tu! Anakwenda mbali zaidi akidai kuwa eti kufunika mwili mzima ni utamaduni wa Wazungu.

Amesisitiza aachwe kwa sababu alichokifanya ni maisha yake na maamuzi yake binafsi. Namwambia wazi kuwa, hajafanya sawasawa na kama anadhani ni maisha yake binafsi basi aachane na muziki.

Kwa taarifa yake, yeye ni mali ya jamii nzima, ni kioo. Jamii inajifunza na kumwangalia yeye. Akikosea lazima aambiwe ukweli.

Kama ni akili yake, ajue alikengeuka na kama alishauriwa basi mshauri wake hakuwa sahihi. Kubwa zaidi na la muhimu kwake, afahamu kuwa mstaarabu akikosea huomba msamaha.

Ustaa siyo kujiachia hovyo. Si kila wanachofanya akina Kim Kardashian na wasanii wetu wa Bongo mfanye. Vingine angalia, kisha endelea na maisha yako ya kibongobongo.

Ni ngumu kuifananisha Bongo na Marekani. Kila kitu tupo tofauti. Nasema kila kitu. Ni kama walivyo tofauti Linna Sanga na Selena Gomez.

Linna badili mtazamo mdogo wangu, vinginevyo mashabiki  waliokupandisha, haohao wanaweza kukushusha wakati wowote. Kazi kwako.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad