Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alitoa kauli tata aliposema amesitisha uchangishaji wa fedha za rambirambi kwa ajili ya msiba mkubwa ulioikumba Shule ya Msingi ya Lucky Vincent.
Wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa shule hiyo walifariki katika ajali ya basi iliyotokea Mei 6.
Mkuu huyo wa mkoa hakufafanua kama alisitisha michango inayopitia ofisi yake au hata ndugu, jamaa na marafiki walioshindwa kutoa pole mapema shuleni na kwa familia za wanafunzi waliofariki.
Tunasema ni kauli tata kwa kuwa Ijumaa iliyopita alitoa amri polisi wakamate na kuwasweka mahabusu watu waliokuwa katika msafara wa meya uliokuwa kwenye shule hiyo kutoa pole. Meya aliongoza msafara wa viongozi wa dini na wa Chama cha Wamiliki wa Shule na vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco) ambao Shule ya Lucky Vincent ni mwanachama wao.
Polisi walisema walipewa amri na mkuu huyo wa mkoa kwa kuwa mkusanyiko huo haukuwa halali na Sh18 milioni walizokuwa wamebeba zilichukuliwa na askari hao na wao wakaswekwa mahabusu. Baada ya meya na wenzake kusota kwa siku mbili mahabusu, ndipo mkuu wa mkoa akatoa tamko la kusitisha uchangishaji rambirambi.
Tunajua wanafunzi hao, walimu pamoja na dereva walifariki dunia njiani baada ya basi walilokuwa wanasafiria kutumbukia kwenye korongo refu. Wanafunzi watatu waliojeruhiwa vibaya wako Marekani kwa matibabu.
Kutokana na idadi hiyo kupotea ghafla kwa wakati mmoja, ulichukuliwa kuwa msiba wa Taifa. Hiyo ndiyo sababu mkuu wa mkoa ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mkoa alichukua jukumu la kusimamia msiba huo ambao Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliongoza wananchi katika kuaga miili ya waliopoteza maisha.
Baadhi ya watu, taasisi, idara na kampuni walipeleka rambirambi zao ofisi ya mkuu wa mkoa, lakini wapo waliopenda kuipa pole shule hiyo moja kwa moja na wengine walikwenda na tunadhani wanaendelea kwenda kuzipa pole familia kwa kuzingatia udugu, ujirani na urafiki.
Misiba, kwa mila na desturi za Tanzania, waombolezaji huchukua siku tatu. Lakini baadhi ya makabila, ikiwa aliyekufa ni mzee mashuhuri katika familia au jamii, huweza kuomboleza mwezi mzima, lengo likiwa kutoa fursa kwa ndugu na jamaa waishio mbali, hata wakifika kuhani baada ya siku tatu za maombolezo wakute watu muhimu hawajatawanyika.
Na ingawa siku tatu za maombolezo kwa msiba wa wanafunzi wa Lucky Vincent zimeisha na wanafunzi ambao hawakuhusika katika ajali wamerejea masomoni, bado kwa utamaduni wa Kiafrika, watu wanaweza kwenda kutoa pole shuleni.
Kwa hiyo, kama tamko hilo linalenga michango inayopitia ofisini kwake atakuwa sahihi. Lakini atakuwa amejitwisha majukumu yasiyo yake kuzuia michango ya watu binafsi, vikundi, wanafunzi wa shule nyingine kwenda kuhani msiba ule.
Tunadhani kwamba hatua yake ya kuwazuia viongozi wa Tamongsco na wadau wengine si sahihi.
Tunamsihi afikirie nje la boksi la siasa na aondokane na dhana potofu kwamba fedha zikipita kwa watu wengine ni ufisadi. Pia atoe ufafanuzi wa kauli hiyo na aeleze ni kiasi gani kilichangwa kupitia ofisi yake na zilitumikaje? Kwa nini posho ya daktari na nesi walioandamana na watoto wagonjwa nchini Marekani wanalipwa kwa fedha za rambirambi badala ya posho za Serikali wakati watumishi hao wako kazini?
Credit Mwananchi