UKWELI Mchungu...Tanzania Ilikua Sahihi Kumtimua Bosi wa UNDP..!!!


Katika Gazeti la RAI toleo la tarehe 4 Mei 2017, kulichapishwa makala yenye kichwa cha maneno : ” Tanzania Ilikuwa Sahihi kumtimua Bosi wa UNDP”. Pamoja na mambo mengine, Mwandishi wa Makala hiyo, Abbas Mwalimu, ameandika kama hivi ifuatavyo:

“APRILI 25 mwaka huu baadhi ya vyombo vya Habari viliripoti taarifa ya kufukuzwa nchini kwa Mwakilishi Mkaazi wa Shirikia la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Balozi Awa Dabo, Serikali ya Tanzania ilimpa saa 24 kurejea kwao.

Ikumbukwe kuwa, Balozi Awa Dabo aliinza kazi ya kuiwakilisha UNDP nchini Tanzania mwaka 2015, hivyo kuondolewa kwake kunahitimisha safari yake aliyoianza tangu kipindi hicho ndani ya Tanzania.

Makala hii fupi inakuletea maelezo ya kidiplomasia kuhusu kufukuzwa kwa Balozi huyo lengo likiwa ni kuondoa mkanganyiko uliojitokeza juu ya uamuzi huo wa Serikali.

Kabla ya kwenda mbali, ni vema na haki kuieleza jamii Balozi ninayemzungumzia hapa ni yupi? Kwa mujibu wa Ibara ya kwanza ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 ambao ulisainiwa mjini Vienna, Austria, mnamo tarehe 18/4/1961 na kuanza kufanya kazi rasmi tarehe 24/4/1961 Balozi ni Mwakilishi aliyetumwa na nchi (Sending State) au shirika au taasisi ya Kimataifa kwenda katika nchi itakayompokea (Receiving State) kwa lengo la kuiwakilisha nchi hiyo au taasisi hiyo au shirika hilo ndani ya nchi hiyo iliyompokea.

Kuna balozi za aina mbili, balozi za kudumu na balozi za nchi na nchi. Balozi za kudumu ni zile zinazofunguliwa na nchi kwenda shirika au taasisi yoyote ya kimataifa, kwa mfano ubalozi wa Tanzania ndani ya New York ambao unaiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Mataifa ni Ubalozi wa Kudumu na Balozi aliyeko kule huitwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania ndani ya Umoja wa Mataifa. Vivyo hivyo Tanzania ina Ubalozi wa kudumu kule Geneva Switzerland.

Kuna Balozi za nchi na nchi ambazo hufunguliwa kwa makubaliano ya nchi husika na kwa mujibu wa ibara ya pili ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961. Ufunguaji huu wa balozi kwa mujibu wa ibara ya pili unahusu pia Balozi za Mashirika na Taasisi za Kimataifa kama vile UN, UNDP, FAO, WHO, ILO n.k. Mabalozi wa mashirika na taasisi za kimataifa wataotumwa na mashirika au taasisi kuwakilisha taasisi hizo au mashirika hayo ndani ya nchi iliyowapokea huitwa Wawakilishi Wakaazi. Ubalozi unaofunguliwa na nchi moja ya Jumuiya ya Madola kwenda nchi nyingine ya Jumuiya hiyo huitwa High Commission wakati ule unaofunguliwa kwenda nchi isiyo ya jumuiya ya madola huitwa Embassy.

Kwa mujibu wa Ibara ya tatu ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, kazi za balozi zimeainishwa kama ifuatavyo;

Kuiwakilisha nchi (Sending State) au shirika au taasisi ya kimataifa iliyomtuma ndani ya nchi husika iliyompokea yaani Receiving State.

Kulinda maslahi ya nchi (dola), taasisi au shirika lililomtuma ndani ya nchi iliyompokea pamoja na raia wake, bila ya kuathiri mipaka aliyowekewa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kujadiliana (ku-negotiate) na serikali ya nchi iliyompokea (Katika mambo mbalimbali yenye maslahi baina yao). Hapa tunaona kuwa Balozi anaweza kusaini mkataba na nchi kwa kumuwakilisha Rais wa nchi husika ambaye amemtuma kumwakilisha ama taasisi husika.

Kuenenda na taratibu zote za kisheria katika kufuatilia yanayojitokeza ndani ya nchi iliyompokea na kutolea taarifa yanayojiri kwa nchi iliyomtuma. Hapa tunaona kuwa mabalozi ndiyo macho na masikio ya marais au wakuu wa Taasisi na mashirika husika yaliyowateua kwenda huko waliko lakini wanatakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata sheria na mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 ambao unawaongoza.

Kuendeleza mahusiano ya kirafiki kati ya shirika au taasisi au nchi iliyomtuma (Sending State) na nchi iliyompokea (Receiving State) sambamba na kuendeleza mahusiano ya kiuchumi, kiutamaduni na kisayansi.

Kimsingi hizo ndizo shughuli anazofanya balozi yeyote kati ya balozi wa kudumu na yule wa nchi na nchi.

JE NCHI ILIYOMPOKEA BALOZI (RECEIVING STATE) INAWEZA KUMSHITAKI BALOZI ALIYETUMWA KATIKA NCHI HIYO?

Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 mabalozi wana Kinga (Immunities) na Upendeleo maalumu (Privileges). Ibara ya 22 ya mkataba inaeleza kuwa maeneo yote ya ubalozi pamoja na vinavyotumiwa ikiwemo magari hayaruhusiwi kuingiliwa ama kupekuliwa na nchi iliyopokea. Ibara ya 23 inaelezea kuhusu mabalozi kutoguswa na kodi zozote zinazochajiwa na nchi husika isipokuwa kwa wale wasiohusika moja kwa moja na ubalozi husika.

Ibara ya 24 inazungumzia kuhusu nyaraka zote za balozi kuwa na kinga ya kukaguliwa, wakati ibara ya 26 inawapa uhuru wa kutembea maneno ya nchi iliyowapokea kwa mujibu wa sheria na mkabata wa Vienna. Ibara ya 27 yenyewe imejikita katika kuelezea kinga ambazo njia zote za mawasiliano kama vile simu, mabegi, mifuko n.k kuwa haziruhusiwi kuingiliwa na ndiyo maana viwanja vya ndege vyote vina sehemu zimeandikwa “Diplomats” ikiwa na maana kuwa ni maalumu kwa ajili ya mabalozi na wafanyakazi wa ubalozi wanaotambuliwa na mkataba wa Vienna wa mwaka 1961. Mkataba umeendelea kuelezea hivyo mpaka ibara ya 30.

Ibara ya 31 ibara ndogo ya kwanza ya mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 inawapa upendeleo mabalozi kutoshitakiwa ama kutohukumiwa na sheria za nchi iliyompokea (Receiving State), isipokuwa;

kwa suala linalohusu mali binafsi isiyohamishika iliyopo ndani ya nchi iliyompokea, isipokuwa labda awe ameishika kwa niaba ya nchi iliyomtuma. Suala lolote au kitu chochote ambacho balozi amekipokea kutoka kwa mtangulizi na ambacho amehusika moja kwa moja kama mtekelezaji ama muongozaji kama mtu binafsi ambacho hakipo kwa niaba ya nchi au taasisi iliyomtuma.

Kama balozi amefanya mambo yanayohusu taaluma ama kibiashara ndani ya nchi iliyompokea nje ya kazi zake za msingi zilizoanishwa kwa mujibu wa mkataba wa Vienna wa mwaka 1961.

Ibara ya 31 ibara ndogo ya pili inawapa upendeleo maalumu mabalozi pia kutotakiwa kutoa maelezo ya ushahidi mahakamani, huku ibara ndogo ya tatu ikifafanua zaidi ibara ndogo ya kwanza (a), (b) na (c).

Kinga na upendeleo anaopewa balozi yeyote unaishia ndani ya nchi alipotumwa tu yaani Receiving State na kinga hizo na upendeleo huo vinaweza kuathiriwa moja kwa moja na nchi ama taasisi iliyomtuma.

Ibara ya 32, Ibara ndogo ya kwanza hapa ndipo penye swali la msingi la swali letu kwamba je nchi iliyompokea balozi inaweza kumshitaki balozi au mwakilishi mkaazi?

Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 kinga wanayopewa ndani ya nchi inayowapokea (Receiving State) ambayo imeelezwa kwenye ibara ya 37 ya mkataba wa Vienna ikielezea kinga zote na upendeleo kwa wafanyakazi wote wa ubalozi na ule wa watu wanaonufaika na kinga hizo ama kwa kuwa sehemu ya familia ama kuwa wafanyakazi wa ubalozi toka nchi iliyowatuma (Sending State) kuanzia ibara ya 29 mpaka ya 36 inaweza kuondolewa na nchi hiyo iliyowatuma tu yaani Sending State. Kwa msingi huo tunaona kuwa nchi iliyomtuma balozi yaani Sending State ndiyo ina wajibu wa kumshitaki ama kuruhusu balozi kushitakiwa baada ya kumuondolea kinga na nchi, shirika ama taasisi hiyo iliyomtuma kuiwakilisha.

ILICHOKIFANYA TANZANIA KWA MUJIBU WA MKATABA WA VIENNA WA MWAKA 1961 UNAOHUSU MAHUSIANO YA KIDIPLOMASIA KINAITWA PERSONA NON GRATA

Niseme tu wazi, hakika nimefurahishwa na Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ndugu Mindi Kasiga alipoulizwa kuhusu sababu za kutomuhitaji mwakilishi mkaazi wa UNDP nchini Tanzania Balozi Awa Dabo alipowaambia waandishi wa habari wawaulize UNDP sababu za kutimuliwa kwa huyo balozi, kwa nini nasema hivi?

Sababu ya msingi ya kufurahishwa nae ni hii; kwa mujibu wa Ibara ya 9 ya Mkataba wa Vienna wa Mwaka 1961 unaohusu mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi na nchi na nchi na mashirika au taasisi za kimataifa inasema hivi:

“Nchi iliyopokea balozi (Receiving State) katika wakati wowote na bila ya kutakiwa kueleza sababu za maamuzi yake, inaweza kuijuza nchi iliyomtuma balozi (Sending State) ama shirika ama taasisi iliyomtuma mwakilishi huyo wa kudumu ndani ya nchi iliyompokea ama mfanyakazi mwingine yeyote aliyeelezwa kwenye mkataba wa Vienna wa 1961 kuwa ni ‘Persona Non Grata’ kwamba mfanyakazi huyo wa ubalozi hakubaliki ndani ya nchi hiyo. 

Neno ‘Persona non grata’ limechukuliwa moja kwa moja kutoka kwenye lugha ya Kilatini ambalo kwa lugha ya Kingereza linaweza kutafsiriwa kama “Person not appreciated” ambapo kwa Kiswahili tunaweza kusema ‘Mtu asiyekubalika ama asiyehitajika’.

Katika hali hiyo nchi au taasisi au shirika lililomtuma balozi linaweza kumrejesha nyumbani ama kuhitimisha shughuli zake za kibalozi. Ifahamike kuwa mtu yeyote aliyeteuliwa kuwa balozi au mfanyakazi wa ubalozi aliyeelezwa kwenye mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 kutoka nchi iliyomtuma ama taasisi ama shirika lililomtuma ndani ya nchi hiyo anaweza kutangazwa kuwa ni ‘Persona Non Grata’ au hakubaliki ndani ya nchi hiyo aliyoteuliwa kwenda bila ya hata kufika kwenye nchi hiyo.

Hapa namaanisha kipindi kile cha uteuzi wa balozi, katika hali ya kawaida watu wengi huwa tunahisi uteuzi wa balozi ni kazi rahisi, la hasha. Kuna mambo mengi huwa yanaangaliwa kama vile lugha, mila na desturi za nchi ambayo balozi anaetarajiwa kuteuliwa n.k. Hivyo katika wakati huu ambapo mawasiliano baina ya nchi hufanyika kwa siri mno baina ya wakuu wa nchi ndipo ambapo napo hali ya persona non grata huweza kujitokeza kutokana na vitu kama hivyo nilivyoeleza.

Ibara hiyo hiyo ya 9 ibara ndogo ya pili inaeleza kuwa, “Kama nchi au taasisi au shirika lililomtuma balozi huyo litagoma au kushindwa kutekeleza jukumu la kumtoa ama kumrejesha Persona Non Grata kama ilivyoelezwa kwenye ibara ndogo ya kwanza nchi iliyompokea inaweza kukataa kumtambua muhusika kama mfanyakazi wa ubalozi husika.

Kwa hiyo basi ninapenda kutumia nafasi hii kwa mara nyingine tena kumpongeza msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ndugu Mindi Kasiga kwa weledi alioonesha katika kuliongelea suala hili nyeti kwa nchi na kwa maslahi ya Taifa, pia napenda kuipongeza serikali yetu kwa kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu katika mahusiano ya kimataifa. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

MAONI: Kwanza napenda kukubaliana na mwandishi wa makala hii, Abbas Abdul Mwalimu, hasa pale aliposema kuwa Nchi inayopeleka (Sending State) inayo haki kabisa ya kumtimua au kumtangaza Balozi au Mwakilishi yoyote yule kutoka Nchi Inayopokea (Receiving State) kuwa ni ‘Persona Non Grata” au mtu asiyetakiwa nchini hata bila ya kuainisha sababu yoyote ile iliyopelekea kuchukuliwa kwa hatua kama hiyo dhidi ya mhusika. Hii ni haki ya kila nchi yenye mamlaka kamili ya kitaifa kufanya itakavyo kuhusiana na masuala kama haya.

Lakini, kuna jambo moja ambalo lazima lifahamike na kuzingatiwa hapa; nalo ni kuwa ukishamtangaza Balozi au Mwakilishi kutoka nchi au Taasisi iliyoko nje ya nchi kuwa hatakiwi nchini, basi ni vyema, kwa serikali ya nchi inayotimua, ikiwa inataka kufanya hivyo, kutoa sababu inayoingia akilini. Nasema hivi kwa sababu unaposema kuwa Balozi au Mwakilishi kutoka nchi au Shirika fulani amepewa saa 24 kuondoka nchini kwa sababu hana maingiliano mazuri na wafanya kazi walio chini yake, hiyo si sababu nzuri na yenye kuingia akilini; kwasababu mwenye uwezo na mamlaka ya kutathmini utendaji kazi mzima wa Balozi au Mwakilishi anayehusika sio Serikali ya Nchi Inayopokea; hiyo ni kazi ya Serikali au Taasisi ya Nchi Inayopeleka.

Kwa lugha nyingine, Nchi Inayopokea inapaswa kujikita zaidi katika kutathmini na kufuatilia kwa karibu maslahi mapana yanayohusiana na mahusiano na mashirikiano ya kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo baina ya Taasisi au Serikali ya Nchi Inayopeleka na Nchi Inayopokea. Na katika hali kama hiyo, Nchi Inayopokea ikiona kuwa vitendo vinavyofanywa na Balozi au Mwakilishi kutoka katika Taasisi au Nchi Inayopeleka vinahatarisha usalama au mahusiano na maingiliano mazuri baina ya pande mbili zinazohusika, basi ni kawaida kabisa kwa Serikali inayohusika kumtaka Balozi au Mwakilishi huyo kuondoka nchini kutokana na vitendo vyake hivyo ambavyo kwa lugha ya kidiplomasia hujuulikana kama “Activities unbecoming or incompatible with his/her diplomatic status”; yaani vitendo vinavyokwenda kinyume kabisa na majukumu yake ya kibalozi.

Ningelipenda kusisitiza hapa jambo moja, nalo ni kuwa bila ya sababu yenye kuingia akilini na kukubalika, si vyema kumfukuza Balozi au Mwakilishi kutoka nchi au taasisi za nje kwa sababu ya kutaka kufukuza au kutimua tu; kwani kufanya hivyo, kunaweza kuleta athari mbaya itakayosababisha Taasisi au Serikali ya Nchi iliyofukuziwa Mwakilishi au Balozi wake nayo kulipiza kisasi kwa kumtimuwa au kumfukuza Balozi au Mwakilishi wa Nchi iliyotimua. Utamaduni huu wa kulipizana kisasi unakubalika kabisa katika ulimwengu wa kidiplomasia na ulikuwa ukifanyika sana wakati wa Vita Baridi baina ya Marekani na Urusi katika miaka ya 60 hadi 80 mpaka pale Ukuta wa Berlin ulipoanguka mnamo mwaka 1989.

La mwisho ambalo ningelipenda kuligusia ni kuwa Mwakilishi wa UNDP, Awa Dabo, hakuwa na cheo cha Ubalozi, na kwa hivyo haikuwa sahihi kumbatiza au kumuita Balozi; kwani vyeo hivi viwili ni tofauti kabisa katika kuzingatia, kulinganisha na kupima darja, hadhi na nyadhifa za kibalozi katika ulimwengu wa kidiplomasia. Kama si zaidi, Awa Dabo alikuwa ni Mwakilishi Mkaazi wa UNDP na sio Balozi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad