UKWELI Mchungu...Vyeti Feki Havikubaliki, Tusioneane Huruma..!!!


Wiki iliyopita ilikuwa ya simanzi kwa baadhi ya watu ambao waliorodheshwa kama watumishi wa umma waliokuwa wanatumia vyeti feki, huku wengine ambao wana vyeti vyao wakilalamika kukuta majina yao katika orodha hiyo.

Ninawapa pole wote ambao wameorodheshwa kimakosa, haki yao bado ipo na watasikilizwa kwa kuwa wana ushahidi wa elimu yao. Hamna haja ya kuwa na wasiwasi kama unajua una sifa na vyeti vyako.

Jambo ambalo halikubaliki ni kwa hawa wengine ambao ama hawana vyeti au wametumia vyeti vya watu wengine kupata ajira katika utumishi wa umma. Orodha ya watu 9,932 iliyotolewa ni kubwa na inaonyesha uozo katika utumishi wa umma.

Baadhi ya watu wamekuwa wakiwaonea huruma watu hao kwa madai kwamba wana watu wanaowategemea. Ni kweli wana wategemezi wao lakini wanasahau kwamba kuna maelfu ya watu wengine ambao wamekosa ajira licha ya kuwa na sifa na elimu ya kutosha.

Hao nao wana ndoto nyingi za maisha na wengine tayari wana familia. Suala la vyeti feki siyo la kuoneana huruma, huu ni wakati wa kurudi kwenye misingi ya utumishi wa umma kwa kuwa na watu wenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na elimu.

Kila nafasi ya kazi inakuwa na kiwango cha elimu ambacho mtumishi anatakiwa kuwa nacho ili kutimiza majukumu hayo. Kuweka mtu asiye na sifa ni kukiuka misingi hiyo ambayo inatuelekeza kufuata weledi katika utendaji kazi.

Huenda tumefika hapa kutokana na kuwa na watendaji ambao hawana sifa na uwezo wa kusimamia masuala ya msingi. Hii ni fursa ya pekee ya kutengeneza mfumo wa utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi na siyo genge la watu wanaotafuta “kula”.

Katika utendaji wa serikali, watumishi ndiyo mashine inaoongoza nchi. Wanasiasa ni kama madereva tu lakini mashine yenyewe ni watumishi wa umma. Kama taifa linakuwa na watumishi wasio na weledi basi hata utendaji kazi utakuwa chini au mbovu.

Tujisahihishe! Ninampongeza Rais Magufuli kwa hatua aliyoichukua kwa sababu inalenga kuimarisha utumishi wa umma nchini. Kila mtu atekeleze majukumu yaliyo ndani ya uwezo wake kulingana na sifa za elimu yake.

Nitakuwa mtu wa mwisho kuwaonea huruma watu hawa eti kwa sababu wana wategemezi. Lazima uamuzi mgumu ufanyike sasa kwa ajili ya manufaa ya badaye ya taifa hili. Na katika uamuzi huo ambao tayari umefanyika, lazima baadhi ya watu wataumia.

Ninaamini mlango mmoja ukufungwa, mwingine utafunguka. Siyo mwisho wa maisha kwa watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma, zipo shughuli nyingi ambazo wanaweza kuzifanya ili kujiongezea kipato mathalani ujasiriamali.

Ombi langu kwa Rais Magufuli ni kufanya mabadiliko ya Katiba ili na viongozi wa kisiasa na wateule wake wachaguliwe kwa kuzingatia elimu yao na siyo tu kujua kusoma na kuandika. Kwa mfano, mtu awe na sifa ya kugombea ubunge akiwa na angalau shahada moja.

Mfumo huo utaongeza uwajibikaji bungeni na kuwafanya wabunge kuwa na upeo mkubwa wa kuhoji mambo bila kuburuzwa na serikali au chama chao. Huo utakuwa ni mwanzo mzuri wa ukombozi wa taifa hili, tayari Kenya wamefanya hivyo.

Tunaamini kwamba wabunge ndiyo watunga sheria, kazi hiyo haiwezi kukamilika kama wabunge hao hawatakuwa na elimu inayowawezesha kuchambua miswada ya sheria, ripoti za ukaguzi wa fedha na bajeti.

Taifa lolote lenye maendeleo linaongozwa na watu wenye elimu. Ukiona kuna ombwe katika uongozi basi chunguza mfumo wa elimu ya nchi hiyo, utabaini kuna kasoro nyingi ambazo zimesababisha mkwamo huo.

Sasa ni wakati kwa serikali kuangalia mfumo wa utoaji elimu ili uwe ambao unamjengea uwezo mwanafunzi. Pia, serikali iweke mazingira magumu kwa watu wanaoghushi vyeti au kutumia vyeti vya wengine.

Kadhalika, serikali iwe na mfumo imara wa kusimamia mchakato wa kuajiri wafanyakazi ili watu wasio na sifa wasipate nafasi ya kuingia kwenye utumishi wa umma. Hii ndiyo misingi itakayoweza kututoa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad