KUTOKA SOBER HOUSE, KIGAMBONI
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Pilli Missanah Foundation, Pilli Missanah, Dogo Mfaume ambaye kwa muda mrefu alikuwa katika kituo hicho akipatiwa matibabu ya kuachana na utumiaji wa madawa ya kulevya, alikimbizwa hospitalini baada ya afya yake kuzidi kuzorota. “Dogo Mfaume alikuwa na matatizo ya uvimbe kichwani kwa muda mrefu, ingawa pia alikuwa akisumbuliwa na magonjwa mengine kiasi kwamba alifikia wakati akashindwa hata kuongea. “Ugonjwa wake ulimsumbua kwa muda wa miezi mitatu, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya tukalazimika kumpeleka Muhimbili kwa matibabu zaidi na kesho (Ijumaa) alikuwa afanyiwe upasuaji huo,” alisema Pili.
DOGO MFAUME NI NANI?
Wakati vijana wenzake wakitamba na Muziki wa Kizazi Kipya maarufu kama Bongo Fleva, Dogo Mfaume aliibuka katikati ya miaka ya 2000 akiimba muziki wa mitaani, ambao ulionekana kama wa kihuni zaidi, wa Mchiriku na
Mnanda, ambako alifanikiwa kujitengenezea jina kubwa baada ya nyimbo zake mbili, Hereni na Kazi yangu ya Dukani kumfikisha kileleni. Mwaka 2009 akiwa katika ubora wake, Dogo Mfaume alitwaa Tuzo ya Msanii Bora wa Muziki Asilia kupitia kibao chake hicho cha Kazi Yangu ya Dukani.
INTERVIEW YA MWISHO NA GLOBAL TV
Miezi michache iliyopita, Dogo Mfaume alifanya mahojiano na Global TV Online, akiwa katika kituo cha kusaidia kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya, Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo alizungumza mambo mbalimbali kuhusiana na safari yake ya matumizi ya madawa ya
kulevya.
JINSI ALIVYOANZA ‘KULA UNGA’
“Mimi nilikuwa navuta bangi tu, sasa siku moja nilikuwa nimekwenda kujiweni nikamkuta mshkaji anavuta, nikamgongea nikijua ni bangi tu ya kawaida. Sasa yule jamaa hakutaka kuniambia ukweli, aliogopa pengine ninaweza kwenda kumtangazia kwa watu na asingeweza kuninyima maana nisingemwelewa. “Kwa hiyo akanipa, nikapiga pafu tatu akaninyang’anya, akavuta tena mara kadhaa akanipa, nikavuta tena, nilipomaliza, nikaona raha f’lani ambayo sijawahi kuiona tangu nianze kuvuta bangi. Nikaanza kama kusinzia hivi kitu ambacho siyo kawaida.”
ATOA UJUMBE MZITO
“Kusema kweli ile raha ilinifanya kesho yake nimtafute yule mshkaji nikamuuliza vipi ile kitu ya jana, akaniambia ili tuipate, inatakiwa buku (shilingi elfu moja) nikampa mia tano na yeye akatoa mia tano, akaenda kuchukua, tukavuta. “Hivyo ndivyo nilivyoanza kuvuta, hii kitu ukianza siyo rahisi kuacha, ndivyo hivyo ilivyokuwa.”
NIMETESEKA MIAKA SABA
“Nimetumia madawa ya kulevya kwa muda wa miaka saba, mwanzo nilikuwa najifichaficha watu wasinione, lakini hali ilivyozidi nikajikuta sioni aibu tena, badala ya kwenda kununuliwa nikawa naenda mwenyewe.”
Wakati mamia ya mashabiki wa Mchiriku nchini wakiamini kuwa Kibao cha Kazi Yangu ya Dukani, kilimpa mafanikio makubwa msanii huyo kimuziki na kimaisha, ukweli kutoka mdomoni mwake ni kuwa wimbo huo ndiyo ulichangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka na hatimaye kuharibika kabisa kwa maisha yake.
“Nilikuwa nimeshaanza kutumia unga wakati natoa kile Kibao cha Kazi Yangu ya Dukani, kusema ukweli wimbo ule ndiyo ulichangia sana kuniangamiza, kwa sababu nilikutana na watu wengi na pia nilipata pesa nyingi, nilikuwa sina mke, sina majukumu, kwa hiyo kadiri nilivyopata pesa ndiyo kasi ya kubwia ilivyozidi
“Kuna siku tulikuwa tumealikwa kwenye shoo sehemu, ilipofika zamu yangu nikaitwa kupanda jukwaani, sasa nilivyoshika mic tu, mtu mmoja aliyekuwa karibu akaanza kupayuka kwa sauti, toa teja hilooo, toa teja hilooo, tumetoa hela yetu hatutaki mateja sisi…Dah! Jamaa alinitoa kabisa kwenye reli, sitakisahau kile kitendo. “Nilimuona jamaa kama ndiyo ananitangazia kwa sababu wakati anasema, alikuwa akisikika katika spika, nikajua Tanzania nzima watajua kama nakula unga maana hadi wakati huo nilitam
bua kuwa hakuna mtu aliyekuwa anajua,” alisema Dogo Mfaume.
Hadi Amani linakwenda mitamboni kulikuwa hakuna taarifa zozote kutoka kwa familia yake, kuhusu msiba na shughuli za mazishi, lakini baadhi ya wasanii wenzake, kupitia mitandao ya kijamii, walizungumzia kifo hicho cha mmoja wa wasanii walioacha alama katika Mchiriku. Wasanii ambao walikuwa wameposti kuhusiana na msiba huo ni pamoja na Mr. Blue, Mheshimiwa Temba, Chegge Chigunda, Nay wa Mitego na Dulla Makabila walionesha kumlilia. Aidha, mitaani hasa uswahili ambako alikuwa na mashabiki wengi kufuatia aina ya muziki aliokuwa akifanya, simanzi imetawala hasa kufuatia taarifa kuwa, ilikuwa arejee kwenye game baada ya afya yake kutengemaa. Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu, Amina. Kwa habari kuhusiana na maisha ya Dogo Mfaume kabla ya kufikwa na mauti.
GPL