KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imekosoa uamuzi wa serikali kuwaajiri madaktari 258 waliokuwa wameomba kwenda kufanya kazi Kenya na kuwaacha mamia ya madaktari ambao hawakuomba na badala yake kusubiri ajira nchini.
Ester Bulaya, akiwasilisha hotuba bungeni mjini hapa jana kwa niaba ya Waziri Kivuli wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel, kuhusu utekelezaji bajeti ya wizara hiyo, alisema wameshangazwa na uamuzi wa serikali kutaka kupeleka madaktari Kenya ilhali kuna uhaba mkubwa wa wataalam hao nchini.
Alisema licha ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kupinga uamuzi wa serikali kupeleka madaktari 500 Kenya, serikali ilipuuza maoni ya chama hicho mpaka pale serikali ya Kenya ilipositisha ombi la uhitaji wa madaktari.
Alisema kitendo kilichofanywa na serikali cha kuipigia debe Kenya huku ikijua dhahiri Tanzania inakabiliwa na uhaba wa wataalamu hao, pengine kuliko Kenya, si cha kizalendo na kimedhihirisha nia mbaya ya serikali kwa wananchi wake wanaoteseka kwa kukosa huduma za afya.
Bulaya ambaye pia Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), alisema pamoja na jambo hilo kukosa uzalendo, mwezi uliopita Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitangaza kuwa Rais ameamuru madaktari 258 walioomba kufanya kazi Kenya waajiriwe nchini mara moja.
“Uamuzi huo si tu umewashangaza Watanzania, bali ulimwengu kwa ujumla. Serikali hii imefanya uamuzi wa ajabu ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi hii tangu uhuru.
Kitendo cha serikali kuwaajiri madaktari walioomba ajira nje ya nchi na kuwatupia kapuni mamia ya madaktari ambao walionyesha uzalendo wa kutamani kuitumia nchi yao ni kitendo cha kibaguzi na kikatili sana kwa wazalendo wa nchi hii," alisema.
Aliongeza kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inapata wasiwasi juu ya uwezo wa serikali katika kuratibu na kupambanua vipaumbele vyake kwa kuwa imeshindwa kujua kama nchi hii ina huduma duni za afya na inakabiliwa na uhaba wa watendaji katika sekta ya afya kuliko Kenya.
Akinukuu ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya Mei, 2016 ya 'Tanzania Service Delivery Indicators', Bulaya alisema inaonyesha utendaji wa sekta ya afya na maendeleo ya sekta hii katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania na Kenya si mzuri.