Usaili wa kazi ni hatua muhimu kwa kila mwenye ndoto ya kuajiriwa na kupata kazi ya ndoto yake. Lakini ni hatua yenye vikwazo vidogo vinavyogeuka kuwa mlima wa kikwazo pale ambapo msailiwa ataruka hatua hizi nne muhimu katika maandalizi yake.
Kutofahamu mambo haya muhimu kabla ya kuingia kwenye usaili, huwafanya wasailiwa wengi kujikuta wakijuta kuingia kwenye usaili husika au kufikiri kuwa hawana bahati ya kupata kazi wanayoitamani kwa kuwa wamejibu vizuri maswali mengi waliyoulizwa.
Lakini maswali unapaswa kufahamu kuwa mambo haya manne yatakupa asilimia zaidi ya 80 ya ushindi kwenye maswali yoyote utakayoulizwa na wasaili. Hata kama maswali utakayoulizwa unayafahamu vilivyo, lakini kushindwa kuyaunganisha na mambo haya kutakuangusha vibaya na huenda ukambilia kudhani ulinyimwa kazi kwa makusudi.\
Fahamu vizuri Kampuni/shirika husika
Hii ni hatua ya kwanza na muhimu sana katika ushindi wa usaili husika. Karibu kila swali utakaloulizwa litakuwa na uhusiano na hili.
Hivyo, unapaswa kufahamu vizuri kazi na huduma au bidhaa zinazotolewa na shirika husika, dhima na dira na lengo kuu la kampuni/shirika hilo. Unapaswa pia kuhakikisha unafahamu washindani wa kampuni husika hususan kama inafanya biashara yoyote.
Tambua Udhaifu, Uimara, Fursa na Hatari/vitisho ambavyo kampuni husika inakutana navyo. Ni rahisi kufahamu mambo hayo endapo utatumia muda wako kufanya utafiti wenye mantiki kuhusu kampuni husika. Taarifa hizi zote unaweza kuzipata kwa kusoma tovuti ya kampuni husika pamoja na machapisho yao mbalimbali.
Hii itakuongezea hali ya kujiamini kwa kuwa unamfahamu vizuri mwajiri wako.
Fahamu kiundani majukumu yote ya nafasi unayowania
Hapa simaanishi tu kukariri majukumu uliyoandikiwa kwenye tangazo la nafasi ya kazi, bali kufahamu kwa kina kinachotegemewa kutoka kwako.
Muajiri wako anatarajia mtu atakayemuajiri awe anajitambua vizuri na amejiandaa kuyakabiri majukumu yake. Anatarajia kuona nia na uwezo wa mtu anayemhitaji kwenye usaili husika.
Ukiyafahamu vizuri majukumu yako na mipaka yake, utakuwa na uwanja mpana wa kujibu maswali yako kwa kumshawishi muajiri kuwa majumu husika unaweza kuyakabili kwa ufanisi zaidi. Kila swali litakaloelekezwa kwako, lijibu ukiwa na picha ya majukumu yako pamoja na kampuni yako.
Kwanini unahitaji kazi hiyo na kwanini unadhani wewe ndiye mhusika
Mwajiri anahitaji sana mtu anayejielewa kama nilivyosema awali, ‘self determined and focused’. Unapaswa kujiuliza vizuri kwanini unahitaji kazi husika, huku ukilizingatia pia swali kuwa unadhani kwanini wewe ndiye mtu unayefaa zaidi kuliko wote.
Kama hufahamu kwanini unahitaji nafasi hiyo, sio kwa sababu unahitaji pesa, hilo linajulikana na ni vyema usiligusie kabisa. Zungumzia upande wa pili wa ‘Career’ yako hasa na unavyotaka kuleta mabadiliko kwenye kazi husika. Ni muda mzuri wa kujinadi.
Ifahamu vizuri, imeze CV yako
Curriculum Vitae (CV), ni maandishi yanayokueleza wewe ulivyo na uhusiano wako na kazi husika. Isome vizuri CV yako baada ya kuandika mambo muhimu unayopaswa kuyaandika. Tutaelezea siku moja kipi hakipaswi kuwekwa lakini huwekwa na wengi.
Usiiache nukta iliyo kwenye CV yako ikupite bila kuielewa vizuri. Isome tena na tena na uelewe kwanini umeandika yote uliyoandika na namna ya kuyaelezea.
Kumbuka katika usaili, CV yako inaweza kuzaa maswali mengi na ikakuinua au kukuangusha. Kumbuka ku-update CV yako kila unapotaka kazi fulani, usiitupe tu kwa kazi yoyote, mengine yanaweza kuwa yanakuinua kwenye kazi A, lakini yakawa chanzo cha kukukoseha kazi B.