“HATUNA jibu mzee huyu atazikwa lini na wapi, lakini mwili wake bado tumeuhifadhi hapa na Serikali inaendelea kuwatafuta ndugu zake halisi ili kujua taratibu za mazishi,” amesema Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mkurugenzi huyo wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Lawrence Mseru alisema hayo jana alipozungumza na HabariLeo na kusisitiza kuwa, mwili wa Mzee Francis Kanyasu maarufu kama Ngosha (86) aliyefahamika hivi karibuni kuwa ndiye aliyebuni Nembo ya Taifa, kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali hiyo hadi watakapopatikana ndugu zake halisi tayari kwa mazishi.
Katika mazungumzo hayo, Profesa Mseru alisema ndugu wa marehemu Ngosha wanatafutwa na serikali kwa kushirikiana na jamaa waliokuwa wakiishi na mzee huyo Buguruni Dar es Salaam. Alisema kwa mujibu wa taarifa alizozitoa Ngosha katika uhai wake, baadhi ya ndugu zake wanaishi Sengerema, hivyo watatafutwa ili watoe kauli kuhusu mazishi ya ndugu yao.
“Wale walioishi na Mzee Ngosha ni jamaa tu waliishi naye, lakini sio ndugu zake halisi… Ni sahihi wana nafasi yao kwa mzee huyo, lakini lazima tuwatafute ndugu zake halisi,” alisema Profesa Mseru.
Kuhusu afya yake, Profesa Mseru alisema kuwa hajakabidhiwa taarifa ya uchunguzi ya mzee huyo kujua alikuwa akikabiliwa na tatizo gani ingawa kwa mujibu wa taarifa ya mwisho iliyotolewa na daktari katika hospitali hiyo, mzee huyo alikuwa na matatizo ya kifua.
Mmoja wa wanafamilia katika familia iliyokuwa ikiishi na Mzee Ngosha, Said Chume, alisema mzee huyo walipozungumza naye Mei 27, mwaka huu aliwataja ndugu zake wawili wanaoishi Sengerema.
“Alitutajia ana ndugu ambao ni Nyanzala Budodi ambaye ni dada yake na John Siang’a ambaye ni mpwa wake. Alisema hao ndugu zake wanaishi Sengerema katika nyumba za Shirika la Nyumba,” alisema Chume.
Familia hiyo ilisema kuwa Mzee Ngosha alikuwa hapendi kwenda hospitali, akiumwa huchuma majani na mizizi ambayo huomba wamtwangie ili anywe na kwamba alikuwa akisumbuliwa na kifua kutokana na uvutaji sigara kwa muda mrefu.
Kabla ya kufariki, mzee huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye ndiye aliyebuni Nembo ya Taifa baada ya kuombwa na Mwalimu Julius Nyerere miaka ya 60 kabla ya uhuru akifanya kazi katika mashamba ya mkonge Tanga...