WAKATI Rais John Magufuli jana akitangaza kuridhia maombi ya kuacha kazi kwa majaji wawili na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, wadau wa sheria wamesema huenda kashfa ya Escrow na dawa za kulevya vinahusika na uamuzi huo.
Ikulu kupitia taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilitoa taarifa jana asubuhi ikieleza kuwa pamoja na Sadiki, Rais aliridhia maombi ya kuacha kazi kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Aloysius Mujulizi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Upendo Msuya, kuanzia Mei 15.
Baada ya habari za kuacha kazi kwa viongozi hao, mijadala ilitawala katika mitandao ya kijamii huku baadhi yao ikihusisha kuacha kazi kwa Jaji Mujulizi kuwa ni kutokana na kuhusishwa na sakata la Escrow ambapo alitajwa miongoni mwa majaji walionufaika kwa kupata mgao.
Kwa mujibu wa ripoti ya Bunge kuhusu sakata la Escrow, Jaji huyo alitajwa kupokea rushwa kwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya IPTL inayoliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wengine waliohusishwa na kashfa hiyo ya kupokea rushwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco na waliokuwa wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge, ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.
Bunge lilitoa maazimio manane yaliyosomwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Zitto alisema mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow yalitumika kuwapa kinachoonekana kuwa ni rushwa.
“Vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya jinai kama vile wizi, ubadhirifu kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi,” alisema.
Alitaja azimio la kwanza la Bunge, ni kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Zitto alisema watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi unaoendelea kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai, watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Azimio la tatu ni kuzitaka kamati husika za kudumu za Bunge, zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge kuwavua nyadhifa zao za uenyeviti wa kamati husika za Bunge.
Zitto alitaja azimio la nne kuwa ni la kumwomba Rais aunde Tume ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa Jaji Msuya uchunguzi wa JAMBO LEO, kutoka vyanzo mbalimbali unaonesha huenda uamuzi wa kuacha kazi kwake unatokana na kuhusishwa na uamuzi wa kesi zake za dawa za kulevya, ingawa taarifa nyingine zinaonesha ugonjwa ndiyo sababu ya hatua hiyo.
Taarifa zinaonesha kwamba Juni 6, 2011 Jaji Msuya alitoa uamuzi wa kuwapa dhamana watuhumiwa wa dawa za kulevya, kwa maelezo kwamba upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha sababu za kuwanyima dhamana, baada ya kukiri kutowasilisha nyaraka muhimu za kutetea hoja zao.
Mwaka 2013, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa amri ya kukamatwa kwa wadhamini wawili wa raia wa Pakistani waliokabiliwa na kesi ya dawa za kulevya kukamatwa.
Uamuzi huo huenda una msukumo wa Jaji Msuya kujiuzulu hasa ikizingatiwa kuwa Rais Magufuli alipata kuzungumzia tabia za baadhi ya watendaji wa Mahakama kuwaachia watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya, hivyo kuzorotesha vita hivyo.
Ikumbukwe, kuwa muda mfupi baada ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga kuapishwa na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam, alisema wapo majaji wanaotoa hukumu kwa kupendelea watuhumiwa hali inayoweka viashiria vya rushwa hivyo kukwamisha mapambano.
“Kazi uliyonipa ni ngumu, kwani mapambano haya yanahusu watu wenye uwezo. Wakati mwingine wanaharibu kesi, ila nakuahidi tutahakikisha tunapambana nao wote wanaohusika,” alisema.
Mawakili
Akizungumzia tukio hilo, Wakili wa Mahakamu Kuu ya Rufaa, Profesa Abdallah Safari alisema ingawa uamuzi huo si wa mara ya kwanza kufanyika, lakini kwa siku za karibuni unaweza kuonekana ni mpya.
Safari alisema mfumo wa majaji unataka kuwepo kwa tume ya kuwaondoa ambao unashirikisha nchi za Jumuiya ya Madola, hivyo inawezekana kulikuwa na fununu ya kufanyika hivyo na wahusika wakaona waondoke kwa heshima kabla ya hatua ya kuwaondoa kuchukuliwa.
“Ninavyowajua, hao majaji bado ni vijana, wana nafasi ya kutumikia Mahakama hivyo kwa hayo ambayo yanasemwa kuwa nyuma yao, yanaweza ndio yamewasukuma kufanya hivyo ili kulinda heshima zao na huko nyuma wengine walishafanya, sitawataja,” alisema.
Kuhusu uwezekano wa majaji hao kushitakiwa kama watakuwa wameachia ngazi kwa misingi ya kashfa, alisema kwa mujibu wa sheria za Mahakama, mtu akifikia sifa ya ujaji analindwa, hivyo hakuna uwezekano huo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu alisema jambo hilo ni la kushangaza: “Hili ni jambo jipya nchini. Huyu Jaji Mujulizi alitajwa kuchota mgawo wa fedha akaunti ya Tegeta Escrow.
“Alitajwa kuchukua fedha katika akaunti hiyo. Kwa nini ameacha kazi sijui! Ila kwa vyovyote vile kitendo cha majaji kuacha kazi licha ya kuwa kinaruhusiwa kikatiba, si cha kawaida sana. Ni vizuri tukapewa taarifa zaidi juu ya sababu za kuacha kazi,” alisema Lissu.
Kuhusu Jaji Msuya, alisema hawezi kumzungumzia kwa kina huku akibainisha kuwa kuacha kazi kwa Meck Sadiki kuna kitu ndani yake.
Lissu alihusisha uamuzi wa Rais Magufuli kumhamishia Kilimanjaro kutoka Dar es Salaam, huku nafasi yake ikichukuliwa na mteule mwingine wa Rais ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.
Lissu alibainisha kuwa TLS itatoa taarifa rasmi ya kuacha kazi kwa majaji hao baada ya kusoma taarifa ya Ikulu na kufanya uchambuzi wa kina.
Wakili wa kujitegemea, Kaloli Mluge alisema hajui ni sababu gani ambayo imefanya majaji hao waache kazi, lakini yeye anadhani maslahi yamepungua na pia ajira serikalini imekuwa ngumu, tofauti na kipindi cha nyuma.
Mluge alisema hivi sasa watu wamechoka kufanya kazi kwa kuburuzwa, kila mtu anafahamu taaluma yake inamtaka afanye nini, kwa hiyo hakuna sababu ya kuanza kumfundisha kazi wakati anajua majukumu yake.
“Ni ngumu kuusemea moyo, lakini mzee kabana sana, maisha yamekuwa magumu serikalini hakuna mtu anayetamani kufanya kazi naye, kutokana na mfumo anaotumia wa kuwafundisha watu wafanye nini,” alisema Mluge.
Wakili Emmanuel Muga alisema njia waliyotumia majaji hao kuacha kazi ni sahihi na pia si jambo la ajabu.
Alisema kila mtu ana uhuru wa kuacha kazi pasipo kuulizwa maswali mengi, kwa sababu hawana makosa na kama wameamua kufanya hivyo ni sawa. Inawezekana wameamua kufanya kazi ya uwakili, ambalo ni jambo zuri tu.
Wakili Abubakar Salim alisema si mara ya kwanza majaji kuacha kazi, watu wamehamaki kwa sababu huko nyuma kulikuwa hakutolewi taarifa ndiyo maana limeonekana kama suala geni.
“Wapo waliokuwa wakiacha kazi kwa uamuzi wao wa kupumzika na kuendelea na maisha mengine. Hii ya leo imeleta maswali mengi kwa sababu tu watu wameona ni tukio jipya, lakini mambo hayo yapo, sema yalikuwa hayatolewi taarifa,” alisema.
Wakili Jamhuri Johnson alisema si jambo geni na kuwa ugeni wake ni kutangazwa katika vyombo vya habari, kitu ambacho huko nyuma hakikufanyika ila sababu za kuacha hawa hatujui.
“Hapa upya ni kutangazwa, lakini majaji wengi wameacha kazi kwa mfano Jaji Chingwile alikuwa Kilimanjaro aliacha kazi, Jaji Kalegea wa Mahakama ya Rufaa aliacha kazi, tatizo ni kutangaza ndicho naona,” alisema.
Kwa sasa haiwezekani hata kupokea rushwa, wakaona isiwe tabu...........wamezoea vya kunyonga, vya kuchinja vimewashinda...HAPA KAZI TU!!!
ReplyDelete