MENGINE mapya yamezidi kuibuka kuhusiana na kuuawa kwa tuhuma za ujambazi mwanafunzi Salum Almas (28) aliyekuwa akisoma stashahada ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) katika Chuo cha Kompyuta (UCC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-
Baada ya ndugu kudai kuwa siku ya tukio alikuwa na Sh. 30,000 alizotumwa azifikishe nyumbani kwao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na polisi kuhusiana na tukio hilo, Almasi aliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Kurasini akituhumiwa kuwa mmoja wa majambazi waliokuwa katika mipango ya kupora zaidi ya Sh. milioni 300 za benki ya CRDB.
Hata hivyo, ndugu zake wamedai kuwa kadri wanavyomfahamu, Salum hakuwahi kujihusisha na vitendo vya aina hiyo na kuomba Serikali ichunguze zaidi kujua ukweli wa kifo chake.
Tukio lililohusisha kuuawa kwake lilitokea Jumapili iliyopita katika eneo la Kurasini, karibu na mahala pa mashine ya kutolea fedha (ATM) ya benki ya CRDB iliyopo jirani na Ofisi ya Uhamiaji.
Mjomba aliyekuwa akiishi na marehemu, Tulleyha Abdulrahman, aliisema kuwa wameshangazwa na madai kuwa kijana huyo alikuwa jambazi na kwamba, wanachoamini ni kuwa polisi walikosea kwa kumdhuru mtu asiyekuwa na hatia.
Alisema anachofahamu ni kwamba siku ya tukio, Salum alikuwa akikatiza maeneo ya benki kuelekea nyumbani kama raia wengine na wala siyo kujihusisha na ujambazi.
“Salum hakuwa kijana wa makundi. Muda mwingi aliutumia kusoma na kuswali. Tunashangaa anaitwa jambazi. Tunamuomba Rais Magufuli aingilie suala hili kwa sababu hiki kilichofanywa na polisi siyo sahihi.
“Wamekatisha uhai wa mtu asiye na hatia. Tunaomba hatua zichukuliwe,” alisema mjomba huyo wa marehemu.
Alisema kinachowaumiza zaidi ni kuona kuwa baada ya tukio hilo, Polisi wametoa kauli zenye utata kwa kudai kuwa marehemu alikuwa katika pikipiki na aliporuka ndipo polisi walipomfyatulia risasi.
Alisema kauli nyingine zilizotolewa ni kwamba wakati wa tukio alikuwa anatembea huku akitangulizwa mbele kama chambo na majambazi wenzake waliokuwa kwenye pikipiki na kwamba, mkanganyiko wa taarifa hiyo ni dalili kwamba kuna utata juu ya kifo cha mwanafunzi huyo na hivyo kuna kila sababu ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina.
Mjomba huyo alisema kuwa yeye alielezwa na polisi kwamba Salum alipita kwenye eneo ambalo lilikuwa likishushwa fedha za kuwekwa kwenye ATM ya benki hiyo na alipoambiwa asimame na askari waliokuwapo na kukaidi, ndipo walipoanza kumpiga risasi.
“Kauli nyingine wanasema Salum alipopigwa risasi ya kwanza aliendelea kutembea akapigwa ya pili hakuonyesha dalili ya kuanguka na alipopigwa ya tatu alidondoka chini na kuanza kutambaa kuelekea eneo ambalo alikuwapo polisi aliyekuwa akimfyatulia risasi,” alisema na kuongeza:
“Wanasema Salum ni jambazi na ni sahihi kilichofanywa na polisi kumuua kwa sababu kama siyo jambazi, mbona aliweza kufanya matendo hayo mpaka kutambaa chini kumfuata polisi mwenye silaha akitaka kumpora,” alisema.
Abdulrahman alisema polisi waliwaeleza kuwa Salum alikuwa na majambazi wenzake waliokuwa kwenye pikipiki lakini jeshi hilo halijaonyesha dalili za kuwatafuta hao wenzake na hiyo ni ishara nyingine juu ya imani yao kuwa kijana wao hakuwa na hatia bali ameuawa kimakosa.
Pia alisema polisi hao waliwaeleza kuwa majambazi walikuwa wamevaa makoti meusi ingawa ndugu yao, siku hiyo alikuwa amevaa kanzu na hata picha zilizopigwa eneo la tukio zilithibitisha kuwa alivaa kanzu.
FEDHA 30,000/-
Abdulrahman alisema familia yake inaishi Kurasini Shimo la Udongo ambako ili mtu afike kituo cha daladala cha JKT, ni lazima apite eneo ilipo ATM ya CRDB.
Alisema kabla ya mauaji hayo majira ya saa 3:33 asubuhi, alizungumza na Salum na kumtaka amfuate kituo cha JKT Mgulani ili amkabidhi fedha na alifanya hivyo.
“Nilionana naye pale kituoni na nilimkabidhi Sh. 30,000 kwa ajili ya kupeleka nyumbani,” alisema.
Alisema baada ya kuachana naye, saa nane baadaye alipigiwa simu na mtu aliyemtaja kwa jina la Sheikh Athuman Juma, akimtaarifu juu ya kifo hicho cha Salum.
“Nilipofika nyumbani nilimuuliza mke wangu kama fedha nilizompa Salum zilifika, akaniambia hapana ndipo nilipobaini muda ambao niliachana naye pale kituoni ndipo alipokwenda kuuawa,” alisema.
Alisema cha kusikitisha ni kwamba alipokwenda kituo cha polisi Chang’ombe na kujitambulisha kuwa ni ndugu wa marehemu, aliambiwa kuwa wanafuga jambazi na hivyo mauaji hayo ni sahihi.
Alisema kuwa alisimuliwa jinsi Salum alivyopigwa risasi hadi alivyotambaa kwa madai kwamba alikuwa akitaka kumpora silaha askari.
Alisema baadaye alikwenda katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke na baada ya kusimulia historia ya Salum, ndipo alipojibiwa kuwa taarifa zake zitazifanyia kazi pamoja na zile za polisi.
Alisema kati ya saa 2:00 na saa 3:00 usiku siku hiyo, polisi walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi na kuchukua kompyuta mbili, flash na daftari la marehemu la chuo.
Alisema vitu hivyo vilikuwa kwenye chumba kimoja ambacho amekitenga kama eneo la kujisomea watoto.
Alisema hivi sasa, maziko yake yatafanyika baada ya taratibu zote kukamilika.
Credit - Nipashe