Wabunge wametoa posho ya siku moja ya kikao kwa ajili ya rambirambi ya vifo vya wanafunzi, walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha.
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema amepata ushauri kutoka kambi zote mbili bungeni kutoa posho yao ya siku moja, fedha ambazo zitagawanywa kwa usawa kwa ndugu wa marehemu wa ajali hiyo.
Kutokana na ushauri huo, ameomba wabunge waamue kuhusu suala hilo jambo ambalo lilikubaliwa na wote.
Kabla ya kuanza kwa shughuli za Bunge leo, wabunge walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka waliofariki dunia katika ajali hiyo.
Wanafunzi 33, walimu wawili na dereva mmoja walikufa katika ajali iliyotokea Jumamosi iliyopita eneo la Rotya wilayani Karatu wakati wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Olasiti jijini Arusha wakienda kufanya mtihani wa ujirani mwema katika Shule ya Tumaini Junior Acadamy.