Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia walimu wawili na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chang’ombe (Mazoezi) kwa tuhuma za kukutwa na mtihani wa Kemia wa kidato cha sita ambayo inaendelea kufanyika nchini.
Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Musa Elius na Innocent Murutu ambao ni walimu wa shule hiyo pamoja na mwanafunzi Ritha Mosha.
Kamishna Sirro alisema wiki iliyopota saa 1:00 usiku Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa Ofisa wa Baraza la Mitihani, Aron Mweteni, aliyesema alimkuta kwenye shule hiyo mwalimu Elius na mtahiniwa wakiwa na karatasi yenye maswali na majibu ya somo la vitendo la kemia.
Alisema baasa ya kuwatilia shaka na baadaye kuwatia mbaroni, walifanya ufuatiliaji wa awli kwa baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambako ilibainika kuwa mtihani huo ni miongoni mwa ile ya kidato cha sita inayofanyika mwaka huu.
“Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na polisi na upelelezi ukikamilika tutawachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani,” alisema Kamishna Sirro.