Jumla Watu 1,945 wamefariki dunia katika ajali za bodaboda 5,418 tangu mwaka 2015 hadi Februari mwaka 2017 hivyo serikali imeanzisha mikakati kabambe ya kupunguza ajali hizo ambazo zinapoteza nguvu kazi ya taifa licha ya kutoa ajira nyingi kwa vijana
Akitoa mikakati ya Serikali jana Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba, amesema kati ya mikakati hiyo ni kupitishwa kwa kanuni ya leseni ya pikipiki na bajaji pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani mashuleni pamoja na vyombo vya habari.
Mhe. Mwigulu amesema kuwa mikakati mingine ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa waendesha bodaboda, kuimarisha usimamizi wa sheria za barabarani pamoja kusisitiza matumizi ya kofia ngumu ili kupunguza madhara pindi ajali zinapotokea.
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kuwa Serikali kupitia wadau mbalimbali nchini pia wanaendesha semina mbalimbali kwa waendesha bodaboda hao ili kupunguza ajali lakini pia amelitaka suala hilo lianzie kuelimishwa kuanzia ngazi ya jamii ili kulidhibiti kabisa.