TAKRIBANI vyeti 700 vya watumishi wa umma viko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa kuhakikiwa upya, kutokana na rufaa zilizokatwa na watumishi hao baada ya Serikali kuruhusu kufanya hivyo.
Taarifa kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) zinaonesha kwamba watumishi wengi waliowasilisha rufani zao ni wenye vyeti vyenye utata visivyokamilika maelezo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa NECTA, John Nchimbi alisema mchakato wa uhakiki wa vyeti hivyo kwa mujibu wa agizo la Rais John Magufuli umemalizika.
Alisema watumishi wengi walijitokeza kukata rufaa na kwamba baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, sasa yanayafanyiwa kazi kisha majibu yatapelekwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Alisema wanajitahidi kuhakikisha rufani na malalamiko ya watumishi hao kuhusu vyeti vyao yanafanyiwa kazi haraka, ili kutoa majibu kwa hatua zaidi za kiutendaji.
“Mwanzoni walikuwa wengi, siwezi kusema kundi kubwa ni akina nani, lakini wengi walioleta ni wa vyeti vyenye utata vinavyotumiwa na watu wengi, pia ambao havijakamilika, lakini wa kughushi ni wachache,” alisema Nchimbi.
Aliongeza kuwa siku ya mwisho iliyowekwa na Rais ilikuwa Mei 15 na kama kuongeza ataongeza mwenyewe na kazi ya Necta ni kutekeleza, hivyo kama kuna fursa basi itatolewa na Rais Magufuli.
Mei 4, Serikali ilitaka watumishi wa umma walioorodheshwa kwenye orodha ya watumishi wa umma wenye vyeti bandia, wakati hawakutakiwa kuwekwa, wakate rufaa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Uhakiki wa vyeti bandia kwa watumishi wa umma, ulihusisha vyeti vya kidato cha nne, cha sita, ualimu na taaluma zingine.
Baada ya uhakiki huo, iliagizwa kuwa watumishi 9,932 waliokuwa na vyeti bandia waondolewe kwenye ajira, watumishi 1,538 wenye vyeti vyenye utata kwa maana kwamba vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, wathibitishe vyeti vyao kabla ya Mei 15 na mishahara yao isimamishwe hadi uhakiki utakapokamilika.
Watumishi 11,596 waliogundulika kuwa na vyeti pungufu, walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao vikaguliwe kabla ya Mei 15, vinginevyo wangechukuliwa hatua.
Aliwataka wanaodai kwamba wamewekwa kwenye orodha ya wenye vyeti bandia wakati hawakutakiwa kuwa huko, kuandika barua za kukata rufaa kwa Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa waajiri wao.
Hata hivyo waajiri hao, walitakiwa kuwasilisha vyeti hivyo Necta kwa ajili ya uhakiki zaidi kabla ya Mei 15.
“Pamoja na hayo, ieleweke kwamba baadhi ya watumishi wakati wanaajiriwa, waliwasilisha vyeti vya matokeo mengine ya sekondari na wakati wa uhakiki, walionesha vyeti vingine.
“Lakini, naomba ieleweke, kwamba hakuna mtumishi wa umma mwenye cheti halali atakayeondolewa katika utumishi wa umma,” alisema.