Waziri wa ardhi,nyumba na Maendeleo ya makazi Mh. William Lukuvi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza,Kiomoni kibamba pamoja na watumishi wa idara ya ardhi na mipango miji,kuacha ubabaishaji katika kusimamia zoezi la urasimishaji wa makazi holela,sambamba na kutoa muda wa siku 7 kwa Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mh. Shanif mansoor kulipa deni la zaidi ya shilingi milioni 500 la kodi ya ardhi analodaiwa tangu mwaka 2010.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo jijini Mwanza wakati akisikiliza kero za wananchi wa kata ya Mahina,ambapo amesema Halmashauri hiyo imekuwa ikiwachukulia hatua za kisheria wananchi wenye maeneo madogo ya ardhi,huku ikiwaacha watu wenye maeneo makubwa ambao wameshindwa kulipa kodi kwa miaka zaidi ya kumi,jambo linaloikosesha mapato serikali na kumtaka Mbunge huyo kulipa deni hilo la shilingi milioni 529 linalotokana na kumiliki eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekta 39 lililopo kata ya Buhongwa ifikapo Mei 5 mwaka huu.
Wakazi wa Mahina wakatoa ya moyoni kuhusiana na urasimu uliopo katika idara ya ardhi jijini Mwanza, yakiwemo malalamiko ya upotevu wa mafaili.
Mh. Lukuvi ambaye yupo katika ziara ya kukagua utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa makazi holela,katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa pia amebaini njama za kutaka kupewa taarifa za uongo na baadhi ya maofisa ardhi wa jiji la Mwanza kuhusiana na suala la viwanja vilivyopimwa.