Alitoa tahadhari hiyo juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati 834 huku viwanja vingine 16,000 vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.
Lukuvi ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa kuandaliwa hati hizo ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina maofisa ardhi na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia hasara Serikali.
Alisema kazi hiyo ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata mapato ya Sh bilioni 2.5 kwa mwaka lakini kilichopatikana ni Sh bilioni 1.3 tu.
“Hakuna halmashauri nchini iliyo na watumishi wengi wa idara ya ardhi kama Ilemela na Nyamagana mara zote nimekuwa nikifikiria kuwahamishia wilaya nyingine kama Geita kwa Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli ambako hakuna hata mmoja.
“Lakini leo pamoja na wingi wenu mnaandaa hati 834 huku viwanja 16,000 mkishindwa kuvikamilisha kwa muda niliotoa.
“Sasa Mkurugenzi nakuambia kwamba Serikali imewavumilia vya kutosha na sasa kama hautabadilika kwa muda ambao nimekuongezea kuanzia sasa hadi Juni 30, mwaka huu tambua kwamba kitambi chako kitapata pancha.
“Wewe mwenyewe utajua namna ya kuiziba pancha hiyo, hatuwezi kuimba wimbo huo huo kila mwaka.
“Kuna vitu vidogo vidogo vya hapa halmashauri mnavifinyia kazi lakini suala ambalo ni la muhimu mnashindwa kukamilisha.
“Nilikuwa namuona mkurugenzi ni mjanja lakini anachokifanya hapa ni kama kutwanga maji kwenye kinu kwa sababu kodi ya ardhi haikusanywi,” alisema.
Waziri alisema Halmashauri za Ilemela na Nyamagana zinatakiwa zikamilishe hatua hiyo Juni 30, mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa baada ya kufungwa urasimishaji makazi haitatokea tena fursa ya namna hiyo.
Alisema wananchi ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli nyingine.
Lukuvi alisema Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu, kazi ambayo itafanywa na wataalamu kutoka China.