ZANZIBAR: Watakaokula Mchana Hadharani Ramadhani Kukiona..!!!


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) imetoa onyo kwa wananchi watakaokula hadharani katika kipindi cha mchana wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma, Khamis Juma Maalim wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua serikali inatoa tahadhari gani kwa watu watakaobainika kula mchana wakati wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema utamaduni wa wananchi wa Zanzibar ni kuheshimu kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa makundi yote ikiwemo wa dini tofauti. Alifahamisha kwamba utamaduni huo upo hata kabla ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 wa dini tofauti kuheshimu dini za watu wengine.

Alisema kazi ya kutoa elimu kuhusu ujio wa mwezi mtukufu wa Ramadhani imeanza kutolewa na Ofisi ya mufti ambayo ndiyo yenye jukumu la kushughulikia masuala ya mambo ya dini ya Kiislamu.

Alisema kazi kama hiyo imeanza kutolewa na maimamu wakuu wa misikiti mbalimbali Unguja na Pemba ikiwemo katika sala za Ijumaa ambazo hukusanya idadi kubwa ya Waislamu kwa wakati mmoja.

Alikiri kuwepo vijana wengi wanaoacha kufunga katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na kula hovyo pamoja na kuvuta sigara. Maalim alisema zipo taarifa kwamba hoteli nyingi hufanya kazi wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo wateja wake wakubwa ni vijana wa Kiislamu. Waislamu nchini wanatazamiwa kuanza mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wiki ijayo ambapo ibada ya funga ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad