Mjamzito anapaswa kuepuka ulaji wa kupita kiasi ili asinenepe kupindukia (Obesity). Kulingana na kijarida kiitwacho Krause’s Food, Nutrition and Diet Therapy, mtoto anayezaliwa akiwa na uzito wa chini sana anakabiliwa na hatari ya kufa mara 40 zaidi kuliko yule aliyezaliwa akiwa na uzito wa kawaida.
Hatari ya kupinda uti wa mgongo inayoletwa na kutoziba kwa mrija wa neva wa kitoto kilicho tumboni, inaweza kuzuiwa iwapo mjamzito ana kiasi cha kutosha cha aina fulani ya vitamini C.
Kwa kuwa mrija huo huziba siku ya 24 hadi ya 28 baada ya mimba kutungwa, baadhi ya wanawake wanaopanga kupata mimba hula vyakula vyenye vitamini hiyo.
Aina hiyo ya vitamini C na madini ya chuma yanaweza kupatikana katika maini, maharage, mboga zenye majani mabichi, njugu na nafaka zilizoongezwa vitamini na madini mbalimbali. Kuchanganya chakula chenye vitamini C, kama matunda yaliyotoka shambani karibuni pamoja na chakula chenye madini ya chuma huongeza madini hayo mwilini.
Kila siku mjamzito anahitaji kula matunda, mboga hasa zilizo na majani ya rangi nzito ya kijani, na zenye rangi ya machungwa, au nyekundu, maharage, soya, dengu na njegere, nafaka kama ngano, mahindi na shayiri—hasa zile ambazo hazijatolewa maganda au zilizotiwa vitu vingine, chakula kinachotokana na wanyama kama samaki, nyama ya kuku, nyama ya ng’ombe, mayai, jibini na maziwa, hasa yale ambayo yametolewa mafuta.
Mafuta, sukari na chumvi vinapaswa kutumiwa kwa kiasi. Mjamzito anywe maji mengi. Aepuke vinywaji vyenye kafeini na vyakula vilivyotiwa dawa za kuhifadhi na kemikali nyinginezo kama za kutia rangi na ladha.
Kuna vitamini ambazo zinaweza kudhuru. Kwa mfano, kiasi kikubwa sana cha vitamini A chaweza kumlemaza mtoto aliye tumboni.
Chuma ni madini muhimu pia. Mwanamke huhitaji madini mengi zaidi ya chuma anapokuwa mjamzito. Asipokuwa na kiasi cha kutosha, damu yake inaweza kuwa na upungufu wa madini hayo. Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi mwanamke apatapo mimba moja baada ya nyingine, kwa kuwa hana nafasi ya kurudisha kiasi kinachohitajika cha madini ya chuma.
Wasichana wenye umri wa chini ya miaka 16 ambao ni wajawazito wanakabiliwa na hatari ya kufa ya asilimia 60 zaidi kuliko wale walio na umri wa miaka 20 na kitu. Kwa upande mwingine, wanawake wenye umri unaozidi miaka 35 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuzaa watoto wenye kasoro, kama vile ugonjwa wa down.
UTUNZAJI WA MIMBA
Utunzaji wa mimba kabla ya kujifungua unaweza kuwasaidia wataalamu kuona hali ambazo huenda zikahitaji utunzaji wa pekee. Hali hizo zinaashiria kuwepo kwa watoto zaidi ya mmoja tumboni, shinikizo la juu la damu, matatizo ya moyo na figo na ugonjwa wa kisukari.
Mwanamke anapaswa kuomba msaada wa kitiba mara moja ikiwa damu inatoka kupitia sehemu ya siri, uso wake unafura ghafla, ana maumivu makali yenye kuendelea kichwani au uchungu kwenye vidole, anapoteza uwezo wake wa kuona ghafla au haoni vizuri, anaumwa na tumbo sana, anatapika sana, anaugua homa, mtoto aliye tumboni anaruka isivyo kawaida, umajimaji unatoka kupitia sehemu ya siri, anasikia maumivu anapokojoa, au hapati mkojo kama kawaida.
Mama anayekunywa pombe na kutumia dawa za kulevya (kutia ndani tumbaku) huzidisha hatari ya kumzaa mtoto aliye na akili pungufu, mlemavu, na hata aliye na tabia yenye kasoro. Mara nyingi wataalamu hupendekeza wajawazito wasiinywe hata kidogo. Wanapaswa pia kuepuka moshi wa sigara.
Ongezeko la uzito linalopendekezwa kwa mwanamke mjamzito ni kilogramu 9 hadi 12 kufikia wakati wa kujifungua. Hata hivyo, wasichana au wanawake ambao hawakuwa wakila chakula cha kutosha wanapaswa kuongeza kati ya kilogramu 12 hadi 15.