Zitto Alishukia Baraza Mawaziri..Ampa Makavu Live Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara..!!!


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amelishukia Baraza la Mawaziri akihoji umakini wake katika kujadili mambo muhimu ukiwamo ustawi wa viwanda na uchumi wa Tanzania.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo huyo ‘aligueka mbogo’ dhidi ya baraza hilo bungeni mjini hapa juzi jioni, alipokuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka ujao wa fedha.

Aliishauri wizara hiyo iangalie upya miradi ya ndani itakayowanufaisha wananchi na kuangalia fungamanisho la kusaidia kuchochea kukaza uchumi.
Zitto pia aliishauri wizara hiyo kushughulikia miradi inayotengeza ajira za ndani ambayo anaamini zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda.

"Hivi Mheshimiwa (Charles) Mwijage mnapokaa katika ‘Cabinet’ (Baraza la Mawaziri), mnajadili  hii mipango. Kwa sababu mkikaa, lazima kuna mtu atasema 'mimi kuna miradi yangu', lakini tunajenga reli, mabehewa yana viti vya ngozi. Hivi mmefikiria namna gani ya kuendeleza zao la katani kuhusu mradi huu?" alihoji.

"Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wako, (Prof. Adolf Mkenda) ni mwalimu wangu wa uchumi mwaka wa tatu, amenifundisha sekta zote za uchumi yaani unachukua, unatafuta njia hii na njia hii, ukiingiza unapata kila kitu. Mimi sitaki kumwambia nimrudishie 'degree' (shahada) yake kwa sababu kwa sasa yeye ndiye Katibu Mkuu katika wizara hivyo anawajibika."

Zitto alisema katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Machi 2016 hadi Machi mwaka huu, bidhaa za viwanda ambazo Tanzania inauza nje, zimeshuka kwa Dola za Kimarekani milioni 500 kutoka Dola bilioni 1.4 mpaka milioni Dola 0.9.

"Tunaposimama hapa na kusema kazi inafanyika, waziri atusaidie kwamba, iwapo kazi inafanyika na kuna ongezeko la uzalishaji, ni kwanini mauzo yetu nje yamepungua kwa kiwango kikubwa? alihoji.

"Na haya ndiyo mambo ambayo ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wazingatie kwa sababu bidhaa za viwanda vinazouzwa nje zinapopungua ni kwamba, viwanda vyetu vya ndani vimepunguza uzalishaji na maana yake kuna watu wamepoteza kazi na kuna mapato ya serikali yanapotea."

Aliendelea kulieleza Bunge kuwa ndani ya miezi 12, Tanzania imepoteza mauzo ya nje kwa Dola milioni 500 na kufikia 2020 anaamini hakutakuwa na senti moja kutokana na mauzo hayo.

Zitto alisema Tanzania ina tatizo kubwa la kulinda viwanda vya ndani ambalo alisisitiza kutokana na bidhaa nyingi za nje kuingizwa nchini kwa magendo.

"Wanaingiza mafuta ya kula kinyemela katika nchi yetu, wanaingiza betri ambazo zinakuwa za bei ndogo na matokeo yake ni kwamba, viwanda vya ndani vinashindwa kushindana nao katika soko," alisema.

Akifafanua kuhusu betri, Zitto alisema takwimu za Idara ya Wateja ya China zinaonyesha kiwango cha betri ambacho kimeingizwa nchini kutoka China katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2016 ni kikubwa, lakini nyingi zimeingizwa kinyemelea.

Alisema takwimu hizo zinaonyesha kati ya Januari na Septemba mwaka jana, betri kutoka China zilizoingizwa nchini zina thamani ya Dola za milioni 36.5.

"Ukija kuangalia kwa Idara yetu ya Forodha hapa nchini, betri ambazo zimeingia nchini na ukalinganisha na TBS (Shirika la Viwango), betri ambazo wamezifanyia ukaguzi zimeingia nchini Dola milioni 5.3, maana yake ni kwamba kuna betri nyingi sana ambazo zinaingia nchini hazipiti katika njia ya kawaida," alisema.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema viwanda vinavyozalisha betri nchini, mfano Panasonic, ambavyo vimeajiri watu, vinashindwa kushindana na vile vya China.

"Tafsiri yake ni kwamba, tutaongea humu kuhusu viwanda na haya ni mambo ambayo tunategemea kuona waziri ukihangaika nayo kwa sababu wahenga walisema bora ndege ambaye unaye mkononi kuliko ambaye yupo juu ya mti," alisema.

"Tuna mradi wa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni saba katika reli. 'Material' (malighafi) yake sehemu kubwa ni chuma, unahitaji tani 50 za chuma cha pua kujenga kilometa moja ya reli. Siyo kwamba hatuna chuma, tunacho Mchuchuma na Liganga.

"Tumewapa Waturuki zabuni ya reli. Wataleta chuma kutoka kwao, ajira zitakwenda kwao. Kabla ya kuanza kufikiria kutandika chuma cha reli, ilitakiwa tuwe tayari tumejenga uwezo wa kuzalisha kule ili fedha zote zibaki kule na ndani ya nchi. Mimi nashindwa kuelewa."

Huku Zitto akishangiliwa na wabunge wa vyama vyote kwa kugonga meza kutokana na mambo ya msingi aliyoyasema katika mchango wake, Waziri Charles Mwijage alimpigia saluti mbunge huyo kuonyesha kukoshwa na mchango wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad