Zitto Kabwe Adai Serikali inaua Viwanda

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameitaka serikali kusimamia ipasavyo sekta ya viwanda ili kuhakikisha kinachozalishwa nchini kinakuwa na maana kwa faida ya Watanzania,


Amehimiza serikali kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya kuvurugwa na bidhaa za nje ambazo zinaingizwa kinyemela, vinginevyo ikubali kuwa inaviua makusudi.

Zitto ambaye ni kiongozi mkuu wa Chama cha ACT –Wazalendo, alisema serikali imekuwa ikishindwa kusimamia ushauri inaopewa na wabunge, akitolea mfano wa alichokieleza bungeni wakati wa mkutano wa bajeti mwaka jana kuhusu umuhimu wa kulindwa viwanda vya ndani.

Alikuwa akichangia hoja ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri Charles Mwijage.

“Wito wangu kwenye hili bado ni uleule, naamini ni muhimu mno kuhakikisha tunaweka utaratibu wa kisera na kisheria wa kulinda bidhaa zetu za ndan. Bado nasisitiza kuwa Serikali iendelee na juhudi za kuhakikisha kuwa tunaongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini,” alisema.

Amesema amekuwa akihimiza viwanda vilivyopo nchini kulindwa na njia nzuri zaidi ya kutekeleza hilo, hususan kwa viwanda vya mafuta ya kula, ni kuzuia uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. “Uzuiaji huu utasisimua uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula, hasa mafuta ya mawese na alizeti,” amesema.

“Kasi ya kulinda viwanda vyetu hivi, inapaswa iwe kubwa na ya haraka sana, bado kuna maeneo yamefichika sana, tukiyakalia kimya kwa sasa madhara yake kwa nchi ni makubwa. Mfano mzuri ni bidhaa ya betri. Kuna smuggling (uingizaji wa bila kulipa kodi/magendo) kubwa ya betri kutoka nje na kuathiri kabisa hata mauzo ya ndani ya viwanda vya betri vilivyopo nchini,” amesema Zitto.

Amegusia kiwanda cha betri cha Panasonic alichosema kimeathiriwa mno na uingizwaji wa betri kutoka nchi za Asia wakati betri hizo hazilipiwi kodi hivyo bei yake kuwa ndogo kuliko betri zinazozalishwa nchini.

Mwenendo huo umesababisha kiwanda cha Panasonic kuwa hatarini kufungwa, hatua itakayolazimu Watanzania wanaofanya kazi hapo kukosa ajira, bali pia na serikali itakosa mapato ya kodi yaliyokuwa yakipatikana kutokana na kiwanda hicho kuzalisha.

“Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya China, mwaka 2016 jumla ya betri zenye thamani ya Dola milioni 36.5 (zaidi ya Sh. milioni 81) zililetwa Tanzania. Lakini kwa upande wa Tanzania, takwimu za TRA na TBS zinaonesha Tanzania iliagiza betri za thamani ya Dola milioni 5.3 tu (wastani wa Sh. bilioni 11) kutoka China,” amesema.

Zitto amesema mtindo huo unamaana kwamba zaidi ya asilimia 80 ya betri zinazoingizwa kutoka nchini China haziingizi kodi. Kwa upande mwingine, ina maana serikali inaruhusu bidhaa za ndani ya nchi kunyimwa fursa ya ushindani wa haki na bidhaa zinazotoka nje ambazo hazilipiwi kodi.

“Jambo hili lina athari kubwa sana kwa Taifa, hasa kwenye mapato ya kodi yanayopotea. Lakini wanaoathirika zaidi ni wazalishaji wa ndani wa betri. Maana bei za bidhaa za magendo ni pungufu zaidi, na hivyo huleta ushindani zaidi kwenye soko,” amesema Zitto ambaye amehimiza ujenzi wa viwanda vipya kwa vile vilivyojengwa zamani haviendesheki mpaka kwanza mifumo yake ya uzalishaji ibadilishwe kutokana na teknnolojia ya sasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad