Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe ametoa ya moyoni kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa zamani wa Moshi mjini kupitia tiketi ya Chadema, mzee Philemon Ndesamburo ambapo pia ametuma salamu za rambirambi kwa mtoto wa mzee huyo.
Mhe. Zitto ametoa salamu hizo leo kwenye ukurasa wake wa faceebook ambapo ameeleza alivyomtambua mzee Ndesamburo.
Salaam zangu za rambirambi Kwa dada yangu mpenzi Lucy Owenya Kwa kupotelewa na baba mzazi Mzee Philemon Kiwelu Ndesamburo. Ni msiba mkubwa Kwa watu wa Kilimanjaro na hasa Moshi Mjini ambapo Mzee Ndesa Pesa alikuwa mwakilishi wake Bungeni kuanzia Mwaka 2000 mpaka Mwaka 2015. Kilimanjaro imepoteza mtu ambaye aliweka maslahi ya mkoa wake mbele kuliko kitu kingine chochote.
Ni msiba mkubwa Kwa wanachama wa CHADEMA ambacho alikuwa Mwenyekiti wake Wa Mkoa tangu Chama kimeanzishwa mpaka mauti yalipomkuta. Huwezi kutaja maendeleo ya CHADEMA kwa nchi yetu bila ya kutaja jina la Mzee Ndesamburo. Nimepata bahati ya kufanya naye kazi Kwa karibu, naweza kutamka bila wasiwasi kwamba ni mmoja wa watu waliokipenda Chama chake Kwa dhati Kabisa.
Ni msiba mkubwa Kwa Watanzania. Mzee Ndesamburo alitumia uwezo wake Wa kifedha na kiakili kuimarisha mfumo wa Vyama vingi nchini kwetu. Mchango wake katika kupigania Demokrasia nchini ni wa kupigiwa mfano na Kwa Kweli wengi wetu Leo tunafaidi matunda ya Vyama vingi Kwa sababu ya kazi kubwa ambayo Mzee Ndesamburo na wenzake walio hai na waliotangulia mbele ya haki walifanya.
Mzee Ndesamburo amechangia Sana ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Kupitia kampuni zake za Keys Hotels ameweza kuchangia Sana ukuaji wa sekta ya Utalii nchini kwetu. Bungeni alikuwa mstari wa mbele kutaka uhifadhi wa mlima Kilimanjaro kutokana na tishio la theluji kuondoka katika uhai wetu ( in our life time). Kwa hakika Vyuo Vikuu vyetu vya Umma vingekuwa vinatenda haki Mzee Huyu angepewa Shahada ya Uzamivu ya Heshima Kwa mchango wake katika Maendeleo ya sekta ya Utalii nchini kwetu.
Nawapa pole Sana watoto, wajukuu na vitukuu vya Mzee Ndesamburo. Mzee wetu aliishi maisha yake na ameacha ‘ legacy ‘ yake. Najua maumivu yenu lakini tupo wengi tunaoumia nanyi. Mungu awavushe kwenye mtihani huu mkubwa. Muwe wamoja na mshikamane.
Poleni Sana ndugu zangu wa CHADEMA Kwa kupotelewa na Kiongozi wenu na Kiongozi wetu pia.
Poleni Sana wana Moshi Mjini na wana Kilimanjaro wote. Poleni Sana Watanzania.
Pumzika Kwa Amani Philemon Kiwelu Ndesamburo. Hiyo ni njia yetu sote. Amina