Kiongozi wa Chama Cha Act-Wazalendo Zitto Kabwe kupitia kumbukumbu ya Makala yake kwenye Gazeti la RAIA MWEMA, JAN 10, 2013
NANI ana miliki ya dhahabu yote iliyogunduliwa Tanzania hivi sasa? Nani ana miliki yote ya misitu iliyopo nchini? Nani ana miliki ya gesi asilia iliyogunduliwa hivi karibuni mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara? Watanzania wachache sana wanayo majawabu ya maswali haya.
Inasikitisha hata Watanzania tuliopewa fursa ya kuwaongoza wenzetu milioni 45 hatuna majawabu na wala hatutafuti majawabu ya swali hili. Viongozi tunawaambia wananchi kwamba “maliasili ya nchi ni mali ya umma.” Ni kweli mali ya umma? Umma ni nani? Hebu tuangalie mfumo wetu wa miliki ya rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia.
Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haisemi lolote kuhusu ‘miliki’ ya utajiri wa taifa. Isipokuwa katika ya kifungu cha tisa (c) na (i) na ibara ya 27 (1) suala la maliasili ya nchi limewekewa masharti ya Katiba.
Ibara ya 9 (c) inasema shughuli za serikali zitatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine. Ibara ya 9(i) inasema matumizi ya utajiri wa taifa yatatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umasikini, ujinga na maradhi.
Ibara ya 27 inahusu wajibu wa raia kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano. Ibara ya 9 kuna masharti ya Katiba ya kujenga Ujamaa. Hakuna ibara ya Katiba inayozungumzia ‘miliki’ ya utajiri wa taifa. Suala hili liliachiwa sheria zilizotungwa na Bunge. Kwa suala utajiri tuliochagua kufanyia kazi katika makala haya sheria hizo ni Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Sheria ya Utafutaji wa Mafuta ya Mwaka 1980.
Nani anamiliki madini nchini?
Sheria ya madini ya mwaka 2010 imesema madini ni mali ya umma, hata hivyo, imeweka masharti ya kuhamisha umiliki huu kwa watu na kampuni binafsi kwa mtindo wa leseni.
Dhahabu ni mali ya umma pale tu utafutaji wake na hatimaye uchimbaji haujatolewa kwa mtu binafsi. Leseni ikishatolewa miliki (mineral right) inahamia kwa mwenye leseni na hapo taifa linabakia kupata mrabaha tu kama tozo ya uvunaji wa rasilimali hii.
Kiuhalisia, mfumo huu unaruhusu maliasili ya nchi kumilikiwa na watu binafsi wawe raia wa Tanzania au la. Angalia mfano huu.
Kampuni iitwayo ZiMinerals LTD kutoka Canada inakuja Dar es Salaam katika Wizara ya Nishati na Madini na kuomba leseni ya kutafuta dhahabu huko Kahama. Wizara inampa leseni ya utafutaji ya mamia ya kilometa za mraba. ZiMinerals inakwenda kujiandikisha katika soko la mitaji la huko Australia na kuanza kukusanya fedha kwa kutumia leseni ya utafutaji dhahabu Tanzania.
Ikishapata fedha inaanza kazi ya kutafuta na baada ya kupata kiwango cha dhahabu wanatangaza na bei ya hisa za kampuni hii zinapanda maradufu. Serikali inaipa kampuni hii leseni ya kuanza kuchimba na kampuni sasa inaanza kuuza dhahabu duniani au inauza miliki hii kwa kampuni nyingine kubwa na yenye uzoefu zaidi au mtaji zaidi.
Kitendo cha ZiMinerals kuuza hisa zake huko Australia tayari miliki ya rasilimali iliyopo Tanzania inakuwa inamilikiwa na wananchi wa nchi hiyo au raia wa nchi nyingine yoyote duniani mwenye kuweza kununua hisa katika soko ambalo hisa za ZiMinerals zinauzwa.
Hivi ndivyo inafanyika. Wanakuja watu hawana hata nguo ya kubadili, wanapata leseni wanakwenda kwao kukopata fedha kwenye masoko ya mitaji na wanakuwa matajiri wakubwa kwa kutumia miliki ya rasilimali za Tanzania na Watanzania wanabaki fukara.
Hivyo ndivyo ilivyofanyika Bulyanhulu, Kampuni ya Sutton Resources ilipewa leseni, ikaenda sokoni kufanyia biashara leseni hiyo, wakawekeza dola za Marekani 20,000 kwenye utafutaji kisha wakauza leseni yao kwa Kampuni ya Barrick Gold, kwa Dola milioni 348. Kwa hiyo tunaposema maliasili hii ni ya taifa tunajidanganya tu. Ukishatoa leseni kinachobaki cha taifa ni ule mrabaha wa asilimia nne tu kwa mujibu wa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 iliyoshinikizwa na sakata la Buzwagi.
Kwa upande wa rasilimali ya gesi asilia na mafuta hali ni tofauti. Miliki ya umma inakuwa ni milki ya serikali na inasimamiwa na Shirika la Umma la Mafuta, hivi sasa TPDC. Kwa hiyo, kwa mfano, kampuni ya ZiGas Limited kutoka Australia inapokuja hapa nchini na kuruhusiwa kutafuta mafuta au gesi na kisha kuchimba, inakua imeajiriwa na TPDC.
Ikienda kule Australia kutafuta fedha itauza kwenye soko ile asilimia yake tu, mara nyingi ni asilimia kati ya 80 na 85. Lakini pia hata ikiuza mafuta au gesi, kulingana na kiwango cha mauzo hayo, asilimia sio chini ya 60 ya mauzo baada ya kuondoa gharama za uzalishaji inachukuliwa na TPDC (serikali).
Hata hivyo tofauti na madini, mrabaha sasa unalipwa na TPDC kwa serikali na sio hii kampuni ambayo ni kama mkandarasi (contractor) wetu. Kwenye gesi tunaweza kusema mali yetu, ingawa si kwa asilimia 100.
Kwa nini mifumo tofauti?
Hakuna maana yoyote ile zaidi ya umazwazwa (ujuha) tu. Kwa nini kampuni za ndani ama za serikali au za watu binafsi haziendi kutafuta fedha kwenye masoko ya mitaji na kufanya utafutaji na kisha kuvuna utajiri huu? Ni ujuha tu maana yote yanawezekana.
Walipokuja Ophir Energy hapa Tanzania na kupata mkataba wa kutafuta mafuta kwenye kitalu namba moja kule Bahari ya kina kirefu mkoani Mtwara, walikwenda kuuza hisa kwenye soko la mitaji na hisa moja ilikuwa inauzwa senti nne ya Pauni ya Uingereza (4 pences). Huu ulikuwa ni mwaka 2006.
Mwaka 2011 baada ya kupata gesi asilia kwenye visima kadhaa, hisa moja ya kampuni hii ilifika senti 654 ya Pauni (654 pences). Licha ya bei kupanda namna hii lakini pia waliuza sehemu ya kampuni yao kwa Kampuni ya BritishGas na kupata mabilioni ya pauni za Uingereza bila Tanzania kupata lolote licha ya biashara hii kuwa ni mali iliyopo Tanzania.
Hivi kweli baadhi yetu tunasimama na kusema gesi asilia mali ya umma? Dhahabu mali ya umma? Almasi mali ya umma? Tunawadanganya wananchi. Lazima kufanya mapinduzi ya kifikra na kivitendo. Maandamano ya watu wa Mtwara yasukume Watanzania kufukua zaidi kuhusu unyonyaji wa utajiri wa nchi. Mapinduzi ni lazima.
Katiba ya nchi sasa iseme kinagaubaga kuwa rasilimali ni mali ya wananchi (sio mali ya umma). Miliki (mineral right) ya utajiri wa nchi iwekwe kwenye mikono ya wananchi wenyewe kwenye maeneo ambayo rasilimali imepatikana au inatafutwa. Serikali itakuwa ni msimamizi wa uvunaji wa rasilimali hii kwa manufaa ya wananchi wote.
Wananchi wa eneo ambalo rasilimali inatafutwa au imepatikana wawe na haki ya kuridhia kuvunwa kwa rasilimali hiyo kabla Serikali Kuu haijatoa ruhusa ya kuvunwa kwa rasilimali hiyo (The right of prior informed consent).
Mapinduzi haya ya umiliki wa rasilimali za nchi kutoka kwa serikali kwenda kwa wananchi wa maeneo yenye rasilimali kutawezesha mrabaha wote unaolipwa na kampuni za uvunaji wa rasilimali kulipwa kwa wananchi hawa kupitia serikali zao za mitaa na majimbo (provinces).
Mapato haya ndio yatafidia kuondolewa kwa wananchi kwenye mashamba yao kupisha uvunaji huu au kufidia samaki wanaopotea kutokana na uchimbaji mafuta na gesi kwenye bahari. Ieleweke kwamba mrabaha si kodi bali ni tozo la fidia kwa kunyonya (kuvuna) mali katika eneo husika.
Viongozi tunaposema maliasili ni mali ya taifa tuna maana fedha zitokanazo na maliasili ni mali za taifa. Hivi tumewahi kujiuliza madhara ya uharibifu wa mazingira nayo ni madhara kwa taifa zima?
Kwa mfano madhara ya kuchimba mafuta kule Mtwara, madhara ya kimazingira ikiwamo sumu yanamilikiwa kwa pamoja kati ya Kigoma na Mtwara au Kigoma itafaidi tu dola zitakazotokana na gesi ya Mtwara lakini Mtwara itaumia peke yake na uharibu mkubwa wa mazingira unaotokana na uchimbaji wa gesi.
Tusiwe na midomo mikubwa kuona fedha za kugawana nchi nzima na kufumbia macho uharibifu mkubwa wa mazingira na upoteaji wa maisha unaowaathiri Watanzania wanaoishi kwenye maeneo fedha hizo zinatoka.
Sumu katika Mto Tigite kule Tarime haigawanywi kwa Watanzania wote isipokuwa mapato ya dhahabu, japo nayo ni kidogo tu maana miliki ni ya kampuni binafsi, inayovunwa na kuchafua maji ya mto huu inagawanywa kwa Watanzania wote.
Hatuwezi kuendelea kuwa na taifa ambalo Wilaya ya Geita yenye mgodi mkubwa zaidi wa dhahabu barani Afrika, ukiondoa Ghana na Afrika Kusini lakini ni masikini zaidi Tanzania. Halafu tunasema maliasili ni mali ya taifa. Turudishe rasilimali kwa wananchi.
Sometimes mpaka nakosa ham hata ya kuishi kwa mijitu kuuza mali zetu na kuchukua chao afu bado wapo mali hii tutairudisha kwa kuwa mmojaaaaaaa WATANZANIA tuamkeeeeeeee
ReplyDelete