Nilishangaa sana baada ya kusoma ujumbe wa Zitto akidai anajuta kuzaliwa Tanzania kwa sababu wabunge hawakumchagua Lawrence Masha kuwa Mbunge wa EALA.
Zitto amesahau kuwa miaka tisa iliyopita alimtuhumu Masha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa anapanga mkakati wa kumfilisi Mzee Reginald Mengi kwa sababu Media zake zilikuwa zinaandika habari za kupinga ufisadi.
Zitto huyu huyu leo eti anajuta kwa nini wabunge hawakumchagua Masha kuwa Mbunge.
Wanasiasa wa Tanzania ni viumbe wa ajabu kweli.
Ninaambatanisha maneno ya Zitto aliyoyasema mwaka 2008 kuhusu Lawrence Masha.
Zitto apasua jina la waziri kijana.
2008-12-07 13:37:18
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema ana ushahidi kuwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha ndiye aliyepeleka hoja ya kumhujumu Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi katika vikao vya juu na kwamba taarifa hizo alithibitisha kuzipata jana.
Akiongea na Nipashe Jumapili jana, Zitto alisema waziri huyo, kwa taarifa alizonazo za kuaminika, alitoa hoja kuwa vyombo vya habari vya IPP vimekuwa mstari wa mbele kupiga vita ufisadi na hii inailetea matatizo serikali.
Hivyo, aliomba serikali ipange mikakati ya kumfilisi Mengi, kitendo ambacho kitasababisha kudhoofishwa kwa vyombo vyake vya habari ambavyo vitashindwa kuendelea kuupinga ufisadi.
Zitto alisema yeye hana sababu ya kumtetea Mengi ila hawezi kunyamaza kuona Mtanzania anayeipenda nchi yake na kulazimika kupinga ufisadi anafanyiwa hujuma.
Aidha, Zitto aliliambia Nipashe Jumapili kwamba, vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuanika maovu ya ufisadi na vyombo hivyo lazima vilindwe na Watanzania wote wazalendo.
Akijibu hoja ya Mengi iliyotolewa jana kuwa yupo tayari kutupwa jela ikithibitishwa kuwa amedanganya na kumwomba Masha pia aseme kama atakuwa tayari kujiuzulu iwapo ukweli wa maneno ya Mengi yatathibitishwa, Masha aliliambia Nipashe Jumapili kuwa hawezi kujiuzulu kwa sababu nia yake ya kuwaagiza polisi kufanya uchunguzi ni kumlinda Mengi.
Alisema kutokana na taarifa ambayo Mengi aliipeleka kituo cha polisi cha Oysterbay, polisi wameamua kuifanyia uchunguzi ili kuhakikisha maisha yake yanakuwa salama.
``Nia ya serikali ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Mengi ni kuhakikisha kuwa tunamlinda,`` alisema Masha na kuongeza kuwa hana tatizo na maneno yaliyotolewa na Zitto ili mradi awe na ushahidi.
Amesema, hata kama hawamuamini, basi waupeleke huo ushahidi kwa Rais au Waziri Mkuu kuuonyesha na kama ikibainika kama ni kweli yeye ndiye anayemhujumu Mengi, basi atajiuzulu.
Akasema kuwa yeye hakusema kuwa atamshughulikia Mengi kama alivyonukuliwa kwenye baadhi ya magazeti ila alisema kuwa sheria itachukua mkondo wake kama ikibainika kuwa tuhuma zilizotolewa ni za kweli.
Akiongea na TBC1 juzi, waziri Masha, alisema kuwa kama Mengi ana ushahidi wa tuhuma alizotoa, serikali haitapata shida ya kuhangaika na ushahidi na imemtaka apeleke ushahidi huo.
Kuibuka kwa sakata hilo kunatokana na Mengi kumtuhumu waziri mmoja kuwa ameagiza abambikiwe kodi bandia ya kiasi kikubwa atakachoshindwa kulipa ili hatimaye afilisiwe.
Alimtuhumu waziri huyo kuwa amekuwa akimtumia ujumbe wa vitisho kutokana na vyombo vyake vya habari kuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele ufisadi.
Akifungua kongamano la kuwajengea uwezo vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa vijana wa chama hicho, John Mnyika, aliwataka vijana kuendeleza vita ya ufisadi na kutokatishwa tamaa na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya watu.
Aliwakumbusha vijana kuwa ni wajibu wao kupigania haki zao kwa manufaa ya taifa na kwamba wanapaswa kukosoana pindi mwenzao anapofanya vibaya.
``Kwa maoni yangu naona kama kauli ya Masha ya kumtaka Mengi awasilishe ushahidi ndani ya siku saba ni ya kukurupuka kwa kuwa mbona nilipotuhumiwa na Mtikila kwamba nimeshiriki kumuua Chacha Wangwe hakusema lolote hadi leo?
Tunashangazwa sana na kauli ya Masha, tulidhani labda angechunguza kwanza kabla hajazungumza na katika hili nawaomba vijana muwe makini na vijana kama hawa na muwakosoe waziwazi,`` alisema.
Alionya kuwa iwapo vijana hawatakosoana jamii itapoteza imani juu ya utendaji wao na kuondoa matumaini ya taifa kuhusu umuhimu wa vijana.
Hata hivyo,alisema vita dhidi ya ufisadi bado ni kubwa kwa kuwa ni asilimia 10 tu imetekelezwa.
``Msibweteke na ushindi huu, ufisadi unaozungumziwa ni wa utawala wa Mkapa, katika awamu ya nne kuna ufisadi kama wa Richmond na Buzwagi kwa hiyo tunapaswa kupambana zaidi,`` alisema.
SOURCE: Nipashe