RAIS wa Shirikisho la Soka (TFF), Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokana na tuhuma za rushwa.
Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, alisema waliwakamata wawili hao juzi kabla ya kuwahoji kwenye ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es Salaam jana.
"Tunaendelea na uchunguzi dhidi yao na viongozi mbalimbali wa TFF," alisema Misalaba.
Hata hivyo, Misalaba alisema kwa sasa hawawezi kuweka wazi kila kitu kwa sababu bado wangali wakiendelea na uchunguzi ambao daima huongozwa na misingi ya sheria.
"Katika uchunguzi wetu tunaongozwa na misingi ya sheria, kanuni na taratibu. Hatuwezi kuweka wazi kila jambo.
"Kikubwa Watanzania waelewe kuwa tuna uchunguzi ambao tumekuwa tukiufanya TFF kwa muda mrefu. Tunawashikilia hao wawili (Malinzi na Mwesigwa) na tunaendelea kuwahoji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Ushahidi tunao, lakini kwamba tutafanya nini, hiyo ni siri ya uchunguzi,” alisema Misalaba.
Pamoja na wawili hao, ofisa huyo wa Takukuru alisema kila kiongozi au mdau wa TFF anayedaiwa kuhusika katika tuhuma hizo za rushwa anachunguzwa, hivyo kuna uwezekano wa kuhojiwa zaidi na hatua kuchukuliwa kadri matokeo ya uchunguzi yatakavyoonyesha.
"Tunafanya uchunguzi wetu kule TFF. Yeyote atakayekuwa amehusika katika ule mkondo, tutamfikia," alisema.
"Kuna tuhuma kule TFF kwamba kuna mambo kadhaa ambayo yamefanyika. Sisi tupo kila mahali na tumejipanga. Hatusubiri kuletewa taarifa tu."
HOJA ZA RIPOTI ZA UKAGUZI
Ingawa Misalaba hakuwa tayari kutaja aina ya rushwa ambayo Malinzi na viongozi wenzake wa TFF wanatuhumiwa, Nipashe inafahamu kwamba kiongozi huyo ni miongoni mwa wadau wa soka waliohusishwa na madai ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti za TFF kinyume cha taratibu hivi karibuni.
Ripoti ya ukaguzi maalum wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa timu ya taifa (Taifa Stars) iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inabainisha hofu ya kuwapo kwa matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi miongoni mwa baadhi ya watendaji wa TFF, akiwamo Malinzi.
Inaelezwa katika ripoti hiyo ambayo uongozi wa juu wa TBL uliithibitishia Nipashe mwezi uliopita kwamba iliandaliwa na Mkaguzi Mkuu wake wa ndani, Richard Magongo, kuwa kati ya Novemba 13, 2013 (siku 11 tangu uongozi wa sasa wa TFF uingie madarakani) na Februari 15, 2014, Dola za Marekani 315,577 (Sh. milioni 688.368) zilitumika bila nyaraka za kuthibitisha matumizi yake kinyume cha makubaliano ya mkataba wa TFF na TBL.
Ripoti hiyo pia inabainisha kuwa kati ya Novemba 11, 2013 na Machi 11, 2014, dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) pia zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaainishwa katika mkataba wa TBL na TFF.
Pia ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha za TFF iliyotolewa Januari 19, mwaka jana na Kampuni ya Ukaguzi ya TAC Associates, inaibua maswali ya kiukaguzi kuhusiana na matumizi ya mamilioni ya shilingi uliofanywa na watendaji wa TFF kwa kushirikiana na wadau wa soka nchini.
Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika Desemba, 2011 uliidhinisha kampuni hiyo kuwa mkaguzi wa nje wa hesabu za shirikisho kwa miaka mitano kuanzia mwaka ulioishia Desemba 31, 2011.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Agosti 15, 2014 hadi Septemba 30, 2015, TFF ililipa jumla ya Sh. milioni 274.072 kwa aliyekuwa Katibu wa Chama cha Soka (FAT sasa TFF), Michael Wambura na kampuni mbalimbali bila kuwa na nyaraka stahiki kuthibitisha malipo hayo.
Mbali na Malinzi, wadau wengine wa soka waliotajwa katika ripoti hizo mbili zenye kuibua maswali kadhaa ya kiukaguzi ni pamoja na Mwesigwa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen.
Mbali na kutofuata matakwa ya Kanuni za Fedha za TFF, ripoti hizo zinabainisha kuwa wadau hao wa soka walipewa fedha hizo bila kukatwa kodi ya serikali, kinyume cha Sheria ya Kodi ya Mwaka 2008.