TANZANIA imepoteza kati ya Sh trilioni 68.6 na Sh trilioni 108.5 tangu kampuni ya Accacia inayochimba dhahabu hapa nchini ilipoanza kusafirisha ‘mchanga wa dhahabu’ nje ya nchi mwaka 1998.
Fedha hizo ni kodi ambayo Serikali ingepata kutoka kwa mwekezaji huyo ambaye ndiye mmiliki wa migodi ya Pangea, Bulyanhulu na Buzwagi ambayo ndiko makinikia yanachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga. Kati ya fedha hizo kwa makadirio ya wastani, Kodi ya mapato ya makampuni ni Sh trilioni 55.67, Kodi ya zuio la kodi bilioni 94.4, Mrabaha Sh trilioni 11.1 na gharama za meli kutia nanga Sh trilioni 1.67.
Makadirio ya juu, Kodi ya mapato ya makampuni Sh trilioni 95.5, Kodi ya zuio la kodi Sh bilioni 94.4, mrabaha Sh trilioni 11.1 na gharama za meli kutia nanga na upakuaji Sh trilioni 1.7. Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Uchumi na Sheria ambayo iliundwa na Rais John Magufuli Profesa Nehemia Osoro, alisema thamani ya madini yote katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi hicho ni kati ya Sh trilioni 183.6 na Sh trilioni 380.5.
“Jumla ya mapato ya Serikali ambayo Serikali ilipoteza ni Sh trillion 68.59 ambazo ni sawa na bajeti ya miaka miwili ya Serikali kwa kigezo cha makadirio ya mwaka 2017/2018. Aidha, robo ya fedha hizo zingetosha kujenga reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Profesa Osoro. Alisema kwa makadirio ya juu Serikali ilipoteza Sh trilion 108.46, ambazo ni sawa na bajeti inayokaribia Miaka Mitatu ya Serikali kwa kigezo cha Makadirio ya Matumizi ya mwaka 2017/2018 na gharama ya kujenga reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Alisema dhahabu peke yake iliyokuwa kwenye kontena moja uzito wake ni kilo 28 na katika makontena 44,277 yatakuwa ni tani 1,240 za dhahabu, kiasi hicho thamani yake ni kati ya Sh trilioni 108.06 na Sh trilioni 183.32. Madini mengine na thamani yake kwenye mabano ni Silver Sh bilioni 329.66 na Sh bilioni 378.3, shaba Sh trilioni 2.86 na Sh trilioni 3.72, Sulphur Sh bilini 227.94 na Sh bilioni 296.9, chuma kati ya Sh bilioni 09 na Sh bilioni 576. Zinc kati ya Sh bilioni 11.6 na Sh bilioni 23.1, Nickel kati ya Sh bilioni 18.3 na Sh bilioni 52.
Madini mengine ni Rhodium, Iridium, Ytterbium, Beryllium, Tantalum na Lithium. Yona, Karamagi walivyohusika Profesa Osoro alimtaja marehemu Dk Abdallah Kigoda kuwa ndiye aliyesaini kwa niaba ya Serikali mkataba na mgodi wa Bulyanhulu ambako Serikali ilipata asilimia 15. Lakini baadaye kwa nyakati tofauti Dk Kigoda alisaini tena mkataba ulioondoa asilimia 10 na baadaye akasaini tena mkataba ulioondoa asilimia 5 ya Serikali.
“Katika marekebisho hayo Serikali ilikubali kulipwa dola za marekani milioni 5 ikiwa ni malipo ya mauzo ya hisa za Serikali,” alisema nakuongeza kuwa Serikali ilikubali kulipwa dola za Marekani 100,000 kwa kila mwaka: “hata hivyo kamati haikuweza kupata uthibitisho wa kufanyika kwa malipo ya jumla ya dola za marekani 6,800, 000 tangu mkataba huo usainiwe.
Kwa upande wa mgodi wa Pangea, aliyesaini ni mkataba huo ni Daniel Yona na Nazir Karamagi Desemba 2003. Alisema katika mikataba hiyo Serikali haina hisa na inatoa nafuu kubwa za kodi kwa mwekezaji jambo ambalo alisema linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato. Mkataba wa mgodi wa North Mara ulisainiwa na Daniel Yona mwaka 1999 na Nazir Karamagi. Alisema katika mkataba wa awali uliosainiwa na Yona ulitoa nafuu ya asilimia 15 ya nyongeza ya mtaji wa kampuni na kuifanya Accacia yakwapua kodi ya trilioni 108/- kampuni hiyo iwe inajilipa kwanza ili kurudisha mtaji wake na asilimia 15 iliyopewa na Serikali.
“Jambo hili lilisababisha kampuni kutangaza hasara katika biashara kila mwaka, jambo hilo limekuwa linaikosesha Serikali kodi ya mapato,” alisema. Mkataba wa mgodi wa Geita ulisainiwa na Dk Abdallah Kigoda na serikali haikupata hisa yoyote. Ngeleja, Chenge watajwa Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mikataba ya uchimbaji madini inaeleza kuwa inaongeza na kurekebisha masharti yaliyomo katika leseni ya uchimbaji madini. Alisema kamati yake inaona kuwa masharti ya aina hiyo ni batili kisheria kwani waziri hawezi kurekebisha masharti ya leseni yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni kwa kupitia vifungu vya mkataba wa uchimbaji wa madini.
Alisema kamati yake imebaini kuwa kumekuwa na uongezaji wa muda wa leseni wa maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria na bila kuzingatia maslahi ya taifa. Alimtaja waziri wa zamani wa madini William Ngeleja na Proresa Sospeter Muhongo ambao waliongeza muda wa leseni kwa kampuni za North Mara na Pangea. Alimtaja aliyekuwa kamishna wa madini Paul Masanja, Peter Kafumu na kaimu kamishna Ally Samaje kuwa walitoa leseni ambazo hazikuwa na maslahi kwa taifa.
Pia aliwataja wakuu wa Serikali kwa masuala ya kisheria kuwa ni Andrew Chenge, John Mwanyika na manaibu wanasheria wakuu ambao ni Felix Mrema na Sazi Salula na wakuu wa idara ya mikataba Maria Ndossi Kejo na Julius Malaba. Kitanzi cha mikataba Profesa Osoro alisema mikataba ya uchimbaji madini ina vifungu thabiti ambavyo vinazuia marekebisho ya sera na sheria kuathiri masharti yaliyomo katika mikataba ya uchimbaji madini. Alisema pamoja na kuwepo vifungu hivyo, Serikali haizuiliwi kurekebisha au kubadili sera na sheria zinazoweza kuathiri mikataba ya uchimbaji madini.
“Mkataba wowote ule hauwezi kisheria kuwa juu ya mamlaka asili ya nchi na maslahi ya umma kuhusu rasilimali zake za asili,” alisema mwenyekiti na kuongeza kuwa mikataba hiyo ina vifungu vinavyoruhusu serikali na makampuni ya uchimbaji kujadili na kurekebisha sharti lolote la kimkataba, hivyo mikataba hiyo inaweza kurekebishika. Misamaha ya kodi Mwenyekiti alisema mikataba ya uchimbaji madini ina vifungu vingi vinavyotoa misamaha mingi ya kodi ambayo haina maslahi kwa taifa. Alisema kwa kutumia mikataba hiyo, makampuni yamekuwa hayalipi kodi kwa kutumia kinga hiyo.
“Inatosha kusema kuwa mikataba hii haina manufaa kwa taifa.” Alisema kitendo cha mikataba kuruhusu fedha zinazotokana na mauzo ya madini kuhamishiwa nje ya nchi, kamati yake iliona kuwa hali hiyo inainyima nchi nafasi ya kukuza uchumi, kuongeza thamani ya fedha yake kutokana na mauzo ya madini kwa sababu fedha haziwekwi katika benki za ndani ya nchi.
“Kamati inaona kuwa utarataibu wa kuweka fedha katika mabenki ya ndani ungewezesha kupunguza mianya ya ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya madini, ni wakati sasa nchi yetu ikaachana na uhuru ambao kampuni za migodi zimepewa ya kuhifadhi fedha zitokanazo na madini nje ya nchi,” alisema Profesa Osoro.
Madaraka ya waziri Kamati hiyo ilisema kuwa sheria ya madini ya sasa inatoa uhuru wa madaraka ya waziri katika kuingia katika mikataba ya madini, hivyo imeshauri mikataba yote mikubwa ya madini inapaswa kupata idhini ya Bunge kama nchi nyingine zinavyofanya. Pia kamati hiyo imeona hakuna sababu ya kupeleka migogoro nje ya nchi kwa ajili ya usikilizwaji na uamuzi ikiwa wahusika katika mikataba hiyo wote ni Watanzania na migodi hiyo ipo Tanzania. mwenyekiti alisema kuna mahakama kuu kitengo cha biashara ambayo ipo kwa ajili ya migogoro kama hiyo