Kampuni ya Madini ya Acacia Yatangaza Kupunguza Wafanyakazi 400

Acacia
Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia imethibitisha kuwa ipo katika mpango wa kupunguza wafanyakazi wake hasa walinzi wa mgodi huo.

Meneja habari na mahusiano ya jamii wa Acacia, Bi. Nectar Foya amesema kuwa kampuni hiyo itaingia mkataba na kampuni binafsi itakayoendesha shughuli za ulinzi wa migodi yake yote mitatu ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi.

Kampuni hiyo imejikuta kwenye msukosuko mkubwa baada Rais John Magufuli kupiga marufuku kusafirisha makontena ya mchanga wa madini kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjua na kuunda kamati ya kuchunguza kiasi cha madini kilichokuwa ndani ya mchanga huo na kujua tathmini ya athari yake kiuchumi.

Kampuni hiyo imetangaza mara kadhaa kuwa zuio hili limewasababishia hasara kubwa. Walisema kuwa wanapata hasara ya dola za Marekani milioni moja (Tsh. bilioni 2.238) kila siku kutokana na katazo hilo la ghafla kutoka kwa serikali.

“Tumeamua kuingia mkataba na kampuni ya ulinzi kwa sababu tunaamini hiyo ndio njia pekee ya kulinda rasilimali zetu na kuzuia tusiendelee kupata hasara,” alisema Bi. foya.

Kauli hii ameitoa baada ya tamko alilotoa Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini Tanzania, Bw. Nicodemus Kajungu mwisho wa wiki iliyopita kwamba kampuni hiyo ipo kwenye mpango wa kupunguza wafanyakazi 400.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sasa hawa jamaa hawaeleweki walisema hayo makontena ni ya mchanga mtupu na wanafanya kazi kwa hasara la kushangaza leo wanasema wanapata hasara ya dollar milioni moja kila siku sasa asieamini kwamba hawa jamaa ni wezi wa kutupwa na wakoloni wabaya zaidi kuwahi kuitawala na kuikandamiza nchi yetu. Huu ni muendelezo wa ukoloni udhalimu wa mtaifa ya magharibi kuendeleza unyonyaji kwa mataifa ya Africa. Hata wakoloni walipoitawala Africa hapo awali waliwatumia vibaraka,waafrica wasiokuwa waaminifu. Na leo tena wanaotuangusha ni hao hao vibaraka wachache kwa tamaa ya maslahi yao binafsi. Ushahidi tunao katika sakata hili la mchanga serikali iangalie uwezekano wa kufungua kesi katika mahakama ya kimataifa japokuwa ni vigumu kwa chui kutenda haki katika kesi ya mbuzi zidi ya simba.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad