Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema jeshi la Polisi katika Mkoa huo linatakiwa kuwa la mfano wa kuigwa katika kukabiliana na kila wimbi la uhalifu, ili wananchi waishi kwa amani kutokana na umuhimu wa biashara.
Makonda ameyasema hayo wakati wa kupeleka magari 26 ya polisi kwenye ukarabati katika gereji iliyoko maeneo ya Utalii mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya matengenzo pamoja na ufungaji wa Kamera katika magari hayo alipokuwa anazungumza na jeshi la polisi leo Osterbay jijini Dar es Salaam.
Amesema katika kukabiliana na rushwa na jeshi hilo, watafunga kamera katika kila kituo ndani ya jiji la Dar es Salaam, ambapo OCD , kanda maalumu, pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi wataweza kuona kile ambacho kinafanyika.
Makonda amesema jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam linatakiwa kuwa la kisasa zaidi katika kukabiliana na uhalifu wa kila namna ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa.
Amesema katika maboresho hayo wataweka Kompyuta kila kituo ili kuachana na kuandika maelezo katika karatasi na mtu yeyote, baada ya kuwekwa kompyuta hizo asikubali kuandikiwa maelezo katika karatasi.
Aidha amesema kuna baiskeli ziko njiani ambazo zitagawiwa kwa polisi ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na uhalifu katika mazingira ambayo kifaa hicho kinaweza kupita.
Nae Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya amesema Jeshi la Polisi kanda maalumu inakabiliwa na changamoto ya magari pamoja na mafuta na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi katika kukabiliana na wahalifu wa kila namna .
Amesema kuwa kutokana maboresho hayo yataweza kubadilisha hata takwimu zilizo katika kipindi hiki zisirudie kutokana na maboresho hayo.