Baada ya Kutumbuliwa..Prof Muhongo ..Mbunge wa Upinzani Ajitokeza Kumteta..!!!

Mjadala wa mchanga wa dhahabu (makinikia) umeibuka tena bungeni mbunge akiwatuhumu wenzake, huku akimtetea Profesa Sospeter Muhongo kuwa ametolewa madarakani kama vile mbuzi wa kafara.

Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea  amesema Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa wawajibike kwa kuwa ni wahusika wa mikataba mibovu ya madini.

Amesema makinikia yana dhahabu lakini yanayofanyika yanaweza kuliingiza Taifa kwenye mgogoro wa kidiplomasia, kisheria na wa kimahakama.

Kubenea ametoa shutuma hizo jana (Ijumaa) akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Amesema Rais John Magufuli amwajibishe pia Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani.

Mbunge huyo amesema hapuuzi nia njema ya Rais Magufuli ya kuwatumikia Watanzania na kuokoa rasilimali za nchi. “Hoja yangu ni kwa nini hatuzungumzii kitendo cha ndege kubwa kubeba dhahabu na tunajadili mchanga, Rais amemtumbua Profesa Muhongo, why (kwa nini) amefanywa mbuzi wa kafara? katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ametumbuliwa, naibu waziri huyu hapa naye awajibike, kwa nini amebaki,” amehoji Kubenea.

Amesema Dk Kalemani amefanya kazi wizarani hapo tangu mwaka 1999 baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo akahoji ni kwa nini asitumbuliwe.


Kubenea amesema Dk Mwakyembe akiwa Wizara ya Katiba na Sheria aliruhusu baadhi ya mikataba mibovu kwa nia ya kumbeba Mwambalaswa.

Mbunge huyo alimzungumzia Bashir Mrindoko, aliyewahi kuwa Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini akisema ni miongoni mwa watu waliotajwa kwamba wanapaswa kuwajibishwa na Rais mwaka 2008 katika ripoti ya Richmond lakini aliendelea na kazi.

“Inashangaza kuona mwaka 2010 huyu  Mrindoko anatoa kibali kwa kampuni ya Singida Wind Power Project iendeshe umeme wa upepo, huyu alikuwa kamishna wa nishati na madini, miongoni mwa watu wanaomiliki hiyo kampuni wamo humu ndani,” amesema.

Amesema wakati kampuni hiyo ikipewa zabuni, Mwambalaswa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na ilibainika baadaye kuwa ni mmoja wa wamiliki.

Mbunge huyo amesema Waziri wa Fedha ndiye anayetoa misamaha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ipo chini yake, lakini waliokuwa viongozi kwenye wizara hiyo wakati huo na sasa wanaendelea kuachwa.

Amesema rekodi zilizopo zinaonyesha mwaka 1993 serikali ilipitisha muswada bungeni wa kuwaruhusu wawekezaji kusafirisha dhahabu, kupata misamaha ya kodi, kuondolewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kuondoa mchanga unaozalishwa na kuusafishia nje.

 “Sasa mheshimiwa spika, mimi sina interest (masilahi) yoyote na Muhongo, kwanza sina mazoea naye hata kusalimiana naye na wala sijazungumza naye lakini katika hili asiwe mbuzi wa kafara, twende mbele zaidi tuangalie wapi tulipojikwaa,” amesema.

Amesema kuna shida kubwa ndani ya serikali kwa kuwa kuna mawaziri au baadhi ya watendaji wakuu wanaokuwa na masilahi katika mikataba na wanakaa kwenye baraza la mawaziri, kumbe nje wana kampuni za mfukoni au za rafiki zao wanaingiza nchi kwenye mgogoro kama Bunge la tisa lilivyopitisha uamuzi mwaka 2008 juu ya Richmond, maazimio hayakutekelezwa kama yalivyotakiwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad