Baada ya vigogo wa Ecrow Takukuru yahamia kwenye Kashfa nyengine


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema itawafikisha mahakamani kutegemeana na ushahidi watuhumiwa wote waliojihusisha na jinai,-


ikiwamo kashfa nyingine nje ya Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo wahusika wake wakuu walinyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwanzoni mwa wiki.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, alisema kuna tuhuma mbalimbali zinazofanyiwa kazi, ikiwamo zilizoainishwa na Bunge.

Nipashe ilitaka kujua hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge nje ya akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwamo utoroshaji wa mabilioni ya fedha kwenda Uswisi, Richmond, Operesheni Tukomeza na North Mara.

"Kosa la jinai haliishi hadi mhusika afariki," alisema Misalaba. "Kama kuna kikwazo, ni suala la muda... uchunguzi ni mchakato mrefu."

"Kesi ya jinai inapokuwapo inachukua muda mrefu. Tunaendelea nayo hadi ushahidi wa kuturidhisha kuwafikisha mahakamani ukamilike.

"Maadamu (mtu) alishatenda jinai, (jambo hilo) halitakwisha hivyo tutawatafuta kokote waliko na hatua stahiki zitachukuliwa.
"Kila tuhuma tunaifanyia kazi."

Jumatatu wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemarila walifikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi, kwa matendo yanayotokana na uchotwaji fedha za akaunti Tegeta Escrow.

Mwaka 2013 Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliwasilisha ripoti ya uchunguzi wa Operesheni Tokomeza na kupendekeza Serikali iwachukulie hatua stahiki za kinidhamu wasaidizi wakuu wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii, walioshiriki katika mpango kazi huo.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwapo mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya maofisa wanyamapori, maofisa misitu katika mapori ya akiba, misitu ya serikali na katika baadhi ya hifadhi za taifa kwa kupokea rushwa, kutesa wananchi, kuwabambikia kesi na kujihusisha na ujangili.

Kufuatia ripoti hiyo, mawaziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii na Mambo ya Ndani ya Nchi walijiuzulu nyadhifa zao.

Maazimio ya Bunge kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow yalifuata mwaka mmoja baadaye.

Katika maazimio hayo ya 2014, Bunge lilitaka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow.

Mei 11, mwaka huu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kwa nini maazimio mbalimbali ya Bunge kuhusu uchukuliwaji wa hatua za kisheria kwa watuhumiwa hayatekelezwi.

Katika swali lake, mbali na kashfa hizo mbili, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai (Chadema) alitaja pia kashfa ya ufichwaji wa mabilioni ya fedha katika akaunti za siri nchini Uswisi.

Lakini sasa, Misalaba amesema masuala yote hayo yapo chini ya uchunguzi wa Takukuru na ushahidi ukipatikana wahusika watafikishwa mahakamani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad