Huwezi Kuamini Haya Ndio Mambo 12 Yaliyowafanya Wabunge Washangilie Bajeti kuu ya Serikali

Bajeti ya Serikali
Mlipuko wa furaha kutoka kwa wabunge uliojitokeza jana wakati Serikali ilipotangaza kufutwa kwa ada ya mwaka ya leseni ya magari (motor vehicle licence), ulitosha kuonyesha ukubwa wa kero hiyo uliokuwapo kwa jamii.

Si kero hiyo tu, kelele za furaha kutoka kwa watunga sheria hao pia zilisikika kwa wingi ilipotangazwa kufutwa kwa ushuru wa usafirishaji wa mazao chini ya tani moja, ushuru wa huduma kwenye nyumba za kulala wageni na kutoza ushuru wa forodha wa asilimia sifuri badala ya 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa mahsusi kwa matumizi ya walemavu.

Zaidi ya mara mbili, Spika wa Bunge, Job Ndugai alilazimika kumtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kurudia alichokisema au kumwambia inatosha na anaweza akaishia hapo kwani wabunge wamemuelewa na hana haja ya kuendelea kuisoma bajeti hiyo.

Ijumaa ya Juni 2, mjadala mkubwa wa kuondolewa kwa ada ya road license uliibuka bungeni, kilio cha wabunge kikiwa ni kuwapo kwa magari ambayo yameegeshwa siku nyingi kutokana na ama ajali au uchakavu wa kutotumika tena hivyo kuitaka Serikali kuifuta ili kuwapa wananchi nafuu na kutoendelea kudaiwa.

Hoja hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni kwenye kipindi cha maswali na majibu ilichangiwa na wabunge wengi akiwamo Spika bila kujali itikadi zao za vyama vyao.

Hapakuwa na majibu ya uhakika siku hiyo kutoka kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ambaye aliishia kusema amelipokea pendekezo hilo na kwamba baada ya kukamilisha taratibu, Serikali itaona hatua sahihi za kuchukua.

Wiki hiyo ikielekea ukingoni, Dk Mpango ametangaza kuifuta sambamba na malimbikizo yake kwa wote waliokuwa wanadaiwa hivyo kuibua nderemo miongoni mwa wabunge hao walioonyesha kufurahishwa baada ya kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa maoni yao. “Serikali inatoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma,” alisema Waziri Mpango.

Bunge lilitawaliwa na kelele za CCM… CCM… CCM mara baada ya waziri huyo pia kutangaza kufuta ushuru kwenye usafirishaji wa mazao yasiyozidi tani moja pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vya walemavu vinavyotengenezwa nchini.

Ilikuwa hivyo pia alipotangaza mpango wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa kutoza asilimia sifuri ya ushuru wa forodha kwenye Mashine za Kielektroni (EFD) kutoka asilimia 10 zilizokuwapo.

Hali ilikuwa hivyo pia ilipotangazwa kuondolewa kwa tozo kwa nyumba za kulala wageni.

Kufutwa kwa ada ya ukaguzi wa viwango ukaguzi wa mionzi na ada ya Wakala wa Vipimo kwenye mbolea ni hatua nyingine iliyowafurahisha wawakilishi hao wa wananchi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad