Chama Cha Mapinduzi (CM) kimewataka viongozi na wote waliotajwa katika sakata la mchanga wa madini kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola baada ya kutuhumiwa kulisababishia Taifa hasara kubwa ya matrilioni ya fedha kutokana na usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam.
Aidha, Polepole alisema kuwa, chama hicho hakitasita kuwachukulia hatua kwa wanachama wake iwapo watabainika kuliingizia taifa hasara kupitia njia mbalimbali ikiwamo hii ya sasa ya kupitia mchanga wa madini. Polepole amesema kwa sasa chama kinaviachia kwanza vyombo vya dola vifanye kazi yake ya kuwahoji waliotajwa kwenye ripoti hizo mbili.
CCM imepongeza Rais Dkt John Pombe Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho kwa jitihada kubwa anazofanya katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinawanufaisha watanzania wote.
Polepole alisema nashangaa kuona baadhi ya wanasisasa na watu wengine wakikejeli hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Rais Magufuli katika kupigania rasilimali za taifa na kusema hatua hizo ni za kihistoria kwani hazijawahi kuonekana popote.
Pamoja na mambo mengine, Polepole amesema kilichofanywa na Rais Magufuli ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo imeelekeza kukomesha wizi unaofanywa na baadhi ya wawekezaji katika migodi ya madini hapa nchini.
Hata hivyo, CCM kimepongeza hatua za awali zilizooneshwa na Mmliki wa Kampuni ya Acacia kwa kukiri kukosea na kuahaidi kufanya mazungumzo na serikali ili kulipa kiasi cha pesa kinachodaiwa na Tanzania.