Chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC) kimetaka vyombo vya dola kuchunguza barua pepe zilizoibua kashfa ya rushwa kati ya familia ya Rais Jacob Zuma na familia ya wafanyabiashara wakubwa nchini humo ya Gupta.
Kwa mujibu wa ANC wameeleza kuwa tuhuma hizo nzito zinapunguza imani na heshima ya serikali yake, hivyo kashfa hizo hazipaswi kuvumilika au kupuuzwa.
Baadhi ya vigogo wa ANC waliungana na upande wa upinzani hivi karibuni wakitaka Rais Zuma ajiuzulu kutokanana na kuandamwa na kashfa za rushwa. Kura za kumtetea zilitosha kumpa nafasi kiongozi huyo kuendelea kuliongoza taifa hilo, huku akiomba radhi kwa kutumia fedha za serikali kukarabati jumba lake kinyume cha sheria.
Hata hivyo, wanasheria wa Zuma wameendelea kupinga vikali kashfa hizo kwa madai kuwa barua pepe zilizovujishwa zilikuwa na mkakati wa kisiasa nyuma yake dhidi ya mteja wao.
Tuhuma za rushwa kati ya familia ya Rais Zuma na familia ya mabilionea ya Gupta zilidai kuwa familia hiyo ya kitajiri imekuwa na nguvu kubwa katika upangaji wa nafasi za uteuzi za Serikali hiyo kwa kutumia uwezo wake wa kifedha.