Dk Mpango Akumbushia Vipaumbele Alivyotoa JPM Wakati Akizindua Bunge..!!!


 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema  bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18 imezingatia vipaumbele 10 vilivyoainishwa na Rais John Magufuli wakati akifungua Bunge la 11 miaka miwili iliyopita.

Akiwasilisha bajeti hiyo leo Alhamisi bungeni mjini Dodoma, amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kujenga uchumi wa kipato cha kati na kutoa unafuu wa maisha kwa wananchi.

Katika eneo hilo Serikali imedhamiria kuongeza mapato, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuimarisha uwajibikaji serikalini.

Pia, eneo lingine ambalo bajeti hiyo imezingatia ni kuhakikisha kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote zilizopita kwa kuweka mifumo imara ya ukusanyaji kodi na kupanua vyanzo vya ukusanyaji wa mapato.

Waziri Mpango ametaja vipaumbele vingine ambavyo ndivyo vinavyoakisi bajeti hiyo kuwa ni kuweka miundombinu ya kisasa kwa kujenga reli na kuimarisha usafiri wa anga na barabara.

“Pia, bajeti hii ambayo imezingatia dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 imetilia maana sekta ya madini kwa kuhakikisha kuwa rasilimali zote zilizopo zinanufaisha Taifa,” alisema.

Bajeti hiyo imetambua umuhimu wa kuendelea kukuza viwanda na imeitambua sekta binafsi kama mbia muhimu ambaye atatoa mchango mkubwa katika kufanikisha mkakati huo.

Uimarishwaji wa sekta ya kilimo cha mazao kwa kuboresha kilimo na uvuvi ni eneo lingine ambalo bajeti hiyo imezingatia.

Dk  Mpango amesema mbali ya maeneo hayo pia bajeti ya safari hii imetilia mkazo eneo la ukuzaji utalii kwa vile limekuwa likitoa mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Huduma za kijamii kama vile afya, maji na elimu yamejitokeza pia kwenye bajeti hiyo yakitajwa kama miongoni mwa vipaumbele ambavyo vitazingatiwa wakati wa utekelezwaji wa bajeti hiyo.

“ Kadhalika bajeti hii imezingatia maeneo kama suala la kupambana na rushwa, dawa za kulevya na mitandao mingine ya kihalifu,” alisema.

Alisema bajeti hiyo pia imezingatia kuleta msukumo mpya wa kiutendaji Serikali ili kwenda sambamba na dhana ya kuwa na taifa la viwanda.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad