Eh..Kumbe Mrisho Ngasa Yupo Yanga kwa Makubaliano Haya Eti..!!!


WINGA aliyekipiga Mbeya City msimu uliopita, Mrisho Ngassa, amerejea kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga na leo amejumuishwa kwenye kikosi hicho kilichocheza na Tusker kwenye michuano ya Super Cup, katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

 Ngassa, ambaye mkataba wake na Mbeya City umemalizika baada ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ameonekana akifanya mazoezi na kikosi cha klabu hiyo ya Jangwani katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam.

Taarifa ambazo BINGWA imezinasa jana kwenye mazoezi hayo, ni kwamba Ngassa ameagizwa kujiweka fiti ili kuangaliwa uwezekano wa kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao.

“Ngassa ameomba kurejea Yanga na benchi la ufundi kupitia uongozi limempa masharti ya kuhakikisha anajifua na kurejesha kiwango chake ili waangalie uwezekano wa kumpa mkataba,” kilisema chanzo hicho.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema michuano hiyo haimzuii mchezaji kutoka timu nyingine kushiriki, bali kikubwa ni kufuata kanuni zao walizoweka.

“Kwa sasa Ngassa yupo na timu yetu akifanya mazoezi na ikibidi anaweza kutumika pia katika michuano hiyo, suala la kumsajili itategemeana na mapendekezo ya kocha, akimhitaji tutampa mkataba,” alisema Mkwasa.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema anachofahamu yeye kuhusu Ngassa ni kwamba amekwenda Yanga kwa ajili ya kufanya mazoezi ili ajiweke fiti na wapo wengine wengi.

“Siyo Ngassa pekee anayefanya mazoezi na Yanga, wapo wachezaji wengi ambao huwezi kuwazuia wala kuwauliza wamefuata nini, kwani kazi yangu ni kufundisha, jukumu la kuuliza nani yupo kwa sababu gani ni la uongozi wa juu,” alisema.

Mbali na Ngassa, wachezaji wengine waliojiunga na kikosi hicho kwenye mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo ya Super Cup ni Babu Ally wa Kagera Sugar, Zahora Pazi (Mbeya City), Haruna Chanongo aliyecheza Mtibwa Sugar msimu uliopita, Emmanuel Kichiba na mshambuliaji mmoja wa Ghana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad