Makusanyo ya tozo mbalimbali za makosa ya usalama barabarani kwa mkoa wa Dar es Salaam yameongezeka kutoka Sh7.3 bilioni hadi Sh12.8 bilioni kwa kipindi cha miezi mitano.
Makusanyo hayo ni ya kati ya Januari na Mei mwaka jana kulinganisha na kipindi kama hicho mwaka huu.
Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya amesema hayo leo (Jumatano) katika hafla ya kukabidhi magari 26 ya doria kwa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya matengenezo.
Amesema kiwango hicho cha faini kinatokana na ongezeko la makosa ya usalama barabarani ambayo kwa kipindi hicho mwaka huu yalikuwa 404,571 kulinganisha na 246,695 mwaka jana.
Mkondya amesema kesi 1,723 za makosa ya usalama barabarani zilifikishwa mahakamani mwaka huu kulinganisha na 1,135 mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la kesi 588 sawa na asilimia 34.
“Ongezeko la makosa ya usalama barabarani ni kutokana na mji kukua kwa kasi na idadi ya watu kuongezeka.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani litaendelea kusimamia sheria na kutaka madereva watii sheria bila shuruti,” amesema.